• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Mtikiso wa nyayo za Raila waangusha dari la PAA Pwani

Mtikiso wa nyayo za Raila waangusha dari la PAA Pwani

NA ALEX KALAMA

CHAMA cha Orange Democratic Movement (ODM) kikiwa kinajivunia kupokea baadhi ya wanasiasa waliohama chama cha Pamoja African Alliance (PAA), uhasimu wa kisiasa baina ya vyama hivyo viwili umeonekana kuzuka upya, pande zote mbili ziking’ang’ania ufwasi wa wapigakura katika Kaunti ya Kilifi.

Kwa miaka mingi, Kilifi imekuwa ngome ya chama cha ODM, na chama cha PAA chenye chimbuko lake katika kaunti hiyo, kimekuwa kwenye harakati kukabiliana na chama hicho na kutwaa ngome hiyo.

Kinara wa chama cha ODM Raila Odinga anafanya ziara yake eneo la Pwani wiki hii, ambapo leo Jumatano anazuru Kilifi.

Mnamo Jumatatu alikuwa katika Kaunti ya Lamu na mnamo Jumanne alikuwa Tana River.

Katika ziara yake ya Kilifi, anatarajiwa kuzindua rasmi shughuli ya usajili wa wanachama wapya wa chama hicho.

Bw Tobias Befondo anayefahamika kwa jina la utani kama Banzi ra Koma ni mmoja wa waliokihama chama cha PAA hivi majuzi na kujiunga na ODM.

Bw Befondo aliambia Taifa Leo kuwa ataendelea kushirikiana na wanasiasa wengine wa chama cha ODM ili kuimarisha ufwasi wake katika Kaunti ya Kilifi.

“Mimi nataka niwaambie watu wa Kilifi chama ambacho kinachoweza kutusaidia sisi ni ODM. Mimi nilikuwa PAA kwa sababu tuliambiwa chama hicho kingesaidia kutatua matatizo yanayotukumba kama wapwani kama vile shida za ardhi lakini kwa mtazamo wangu hiyo ilikuwa hadaa tupu. Sikujua mapema kwamba wengine walikuwa wanatutumia kama ngazi kutimiza ajenda zao za kibinafsi,” akasema Bw Befondo.

Bw Befondo aliwania kiti cha uwakilishi wadi Kisurutini mwaka 2022 kupitia chama cha PAA na kuangushwa na mwakilishi wadi wa eneo hilo Mae Mwadena wa chama cha ODM.

Wakati huo huo mbunge wa Rabai Anthony Kenga Mupe amepuuzilia mbali siasa za vyama na kuwataka viongozi kuwatumikia wananchi badala ya kuendeleza siasa.

“Huu si wakati wa kufanya siasa za vyama kukiwa na shida nyingi ambazo zinakumba wakazi wa Kilifi. Kile cha muhimu kwa sasa ni kuangalia vile tutaweza kushirikiana na kutatua hizi shida. Wananchi hawa walituchagua sisi ili tuwatumikie… hawakutuchagua ili tutumikie chama. Ukweli ni kwamba wengi wetu tulichaguliwa kupitia vyama ila kwa sasa lazima tuwape kipaumbele wananchi halafu mambo ya vyama yaje baadaye,” akasema Bw Mupe.

Aidha Bw Mupe ameashiria kufanya uamuzi wa chama atakachotumia kupigania kiti chake ifikapo mwaka 2026.

  • Tags

You can share this post!

Raia wawili wa Nigeria wazuiliwa kwa kuilaghai Text Book...

Karibisheni watoto chokoraa wanaorandaranda majumbani...

T L