• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Mudavadi apeleka waraka wa habari njema Nyanza

Mudavadi apeleka waraka wa habari njema Nyanza

KASSIM ADINASI Na BENSON MATHEKA

MKUU wa Mawaziri Musalia Mudavadi amedokeza uwezekano wa kufanyika kwa handisheki kati ya Rais William Ruto na kiongozi wa Azimio la Umoja-One Kenya Raila Odinga.

Akizungumza akiwa Bondo, Kaunti ya Siaya nyumbani kwa Bw Odinga mwishoni mwa wiki, Bw Mudavadi alisema kuwa “kuna habari zuri na za kipekee kwa wakazi wa Bondo (Nyanza)”, kauli iliyopokelewa kwa furaha na umati uliohudhuria hafla ya kanisa la ACK aliyoshiriki kama mgeni wa heshima.

“Ninawaomba mniangalie vizuri. Hivi karibuni tutawashangaza kwa habari njema, za kupendeza na muhimu. Nakili tarehe hii na mahali ambapo nimezungumzia jambo hili. Sitaki nitoboe sana kulihusu jambo hilo,” alisema Mudavadi.

Ujumbe huu kwa watu wa Bondo na eneo la Nyanza kwa jumla unafasiriwa kama ishara ya ujio wa handisheki kati ya Bw Odinga na Rais Ruto au huenda kiongozi huyo wa ODM akapewa kazi katika Umoja wa Afrika (AU) .

Kumekuwa na tetesi kuwa huenda Bw Odinga anapigiwa debe kuwa mwenyekiti wa Tume ya AU, wadhifa ambao haujawahi kushikiliwa na Mkenya.

Wadhifa huo utabaki wazi baada ya muhula wa Moussa Faki wa Chad kukamilika mwaka 2025.

Hii, kwa namna fulani, inaweza kuwa hatua ya kudhoofisha zaidi muungano wa Azimio ambao tayari unakumbwa na mgawanyiko huku baadhi ya viongozi wake wakitofautiana.

Ni dhoruba ambayo huenda ikatikisa na kusambaratisha muungano wa upinzani baada ya ripoti ya NADCO ambayo Bw Odinga aliidhinisha ikikataliwa na baadhi ya vinara wenza wa Azimio.

Iwapo Rais Ruto atamwidhinisha Bw Odinga kwa kazi ya Bara, hali ya siasa itabadilika nchini kwa kumwondoa waziri mkuu huyo wa zamani nje ya uchaguzi mkuu wa 2027 na hivyo kufanya vigogo wa Azimio kubuni mkondo mpya.

Wachambuzi wa siasa wanataja tamko la Mudavadi kama la kisiasa wakisema handisheki ya Dkt Ruto na Bw Odinga itakuwa pigo kwa kiongozi huyo wa upinzani.

“Dkt Ruto amekuwa akisisitiza mara si moja kwamba hawezi kukaribisha upinzani katika serikali yake. Amekuwa akiutaka upinzani kutekeleza jukumu lake la kukosoa serikali na hata kupendekeza afisi ya kiongozi rasmi wa upinzani. Hii inaondoa uwezekano wa kuridhiana kisiasa na Bw Odinga isipokuwa kwa shinikizo kutoka mataifa ya Magharibi yanayofadhili serikali,” asema mdadisi wa siasa Dkt Isaac Gichuki.

Anaongeza: “Handisheki ya Ruto na Odinga inaweza kuwa pigo kwa Mudavadi mwenyewe na sidhani alikuwa akimaanisha hivyo japo siasa ni telezi. Kenya Kwanza imekuwa ikirushia minofu ngome za Raila na sitashangaa ikiwa alimaanisha hivyo kwa watu wa Bondo.”

Hata hivyo, alisema Rais Ruto anaweza kufurahia sana Bw Odinga akiondoka katika siasa za Kenya hasa uchaguzi mkuu wa 2027.

“Iwapo anaweza kumshawishi Raila kutwaa wadhifa huo, kwa njia moja atakuwa amemwondoa katika kinyang’anyiro cha 2027 na kufanya Azimio kuwa gae,” akasema na kuongeza kuwa Bw Odinga anaonekana kujiandaa kwa uchaguzi japo hajatangaza azma ya kuwania urais kwa mara ya sita.

Kwa upande mwingine, Bw Mudavadi alitoa wito kwa wapigakura wa eneobunge la Bondo kujinufaisha kwa fursa ya uuzaji wa bidhaa katika soko la Muungano wa Ulaya bila ushuru na masharti magumu.

“Ningependa kuwaambia kwamba kupitia Bw Alfred Kombudo ambaye ni Katibu wa Biashara, kama nchi, tumepata soko la Muungano wa Ulaya. Ni lazima sasa tukumbatie fursa inayotokana na uuzaji nje wa bidhaa bila kutozwa ushuru,” akasema Bw Mudavadi.

  • Tags

You can share this post!

NHIF imeoza kwa ufisadi – Nakhumicha

Kundi la ufundi wa chumbani lashangaza wanaume

T L