Siasa

Muungano wa viongozi kina mama kumpigania Gachagua

May 22nd, 2024 1 min read

NA MWANGI MUIRURI

MUUNGANO wa viongozi wanawake katika ukanda wa Mlima Kenya umeapa kumkinga Naibu Rais Rigathi Gachagua dhidi ya kile wamedai ni mashambulio na vita vya kisiasa.

Muungano huo umesema utadhihirishia mahasidi wote wa kisiasa wa Bw Gachagua kwamba “licha ya kutuona tumevalia marinda, tuko vingine kwa umbo na tuko sawa na wanaume”.

Mbunge wa Maragua Bi Mary Wamaua akihutubu Jumanne katika Kaunti ya Kirinyaga, alisema kwamba hata wanaompiga Bw Gachagua vita ni vijitoto vya kisiasa na visivyo na mashiko wala makali.

“Hao sisi viongozi wanawake wa Mlima Kenya tutawakabili vilivyo,” akasema Bi Wamaua.

Bi Wamaua alisema liwe liwalo Mlima Kenya watazama au wainuke na Bw Gachagua.

“Wenye mawazo tofauti wajue kwamba watakumbana na hasira ya wazazi wa kunyonyesha,” akaongeza.

Alisema wao ndio walizaa wadhifa wa Bw Gachagua kwa kura zao.

“Ni sawa na kuzaa mtoto. Aujuaye uchungu wa kuzaa ni mama mzazi. Mama ndiye huhisi uchungu wa miezi tisa hadi kuzaa mtoto. Sawa na hilo la uzazi, ifahamike tuko katika awamu ya kulea wadhifa wa Bw Gachagua na hilo tutalifanya kwa kujitolea,” akasema.

Wanachama wa muungano huo ambao wamekiri hadharani ni Mbunge wa Naivasha Bi Jane Kihara, Seneta Maalum Veronica Maina, Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Kirinyaga Bi Njeri Maina, Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Nyeri Bi Rahab Mukami pamoja na Mbunge maalum Bi Sabina Chege.

Bi Maina alidai kwamba ikiwa wenyeji wa Mlima Kenya wangechagua muungano wa Azimio La Umoja-One Kenya “sasa hivi tungekuwa kwa mtaro kama nchi”.

“Bw Gachagua ni mzalendo na shujaa wa kijamii. Wanaomtikisa wajue wanajaribu kutikisa Mlima. Tuko tu hapa hatujasonga,” akasema Bi Maina.

Bw Gachagua na Rais William Ruto walichaguliwa kupitia kwa tiketi ya muungano wa Kenya Kwanza. Wote wawili ni wanachama wa chama cha United Democratic Alliance (UDA).