• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 8:50 AM
Mvutano wa Wetang’ula na Natembeya waanza kutoa usaha

Mvutano wa Wetang’ula na Natembeya waanza kutoa usaha

NA EVANS JAOLA

MAAFISA wanne wa serikali ya Kaunti ya Trans Nzoia mnamo Jumanne walihojiwa katika makao makuu ya Idara ya Kuchunguza Makosa ya Jinai (DCI) katika kaunti hiyo, kutokana na ghasia zilizotokea kwenye hafla moja ya mazishi Ijumaa iliyopita.

Mazishi hayo yalikuwa yamehudhuriwa na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula na Gavana wa Kaunti ya Trans Nzoia George Natembeya.

Wanne hao wanajumuisha msaidizi wa kibinafsi wa Bw Natembeya na Mkurugenzi wa Idara ya Kushinikiza Uzingatiaji wa Sheria za Kaunti, Bw Frederick Ndubi.

Wengine waliohojiwa ni diwani wa zamani wa wadi ya Kapomboi, Bw Bernard Wanjala, almaarufu ‘Mulipoko’, ambaye ni mshirika wa karibu wa Bw Wetang’ula.

Maafisa hao walihojiwa kwa zaidi ya saa tatu, kuhusiana na tuhuma za kupanga na kufadhili ghasia hizo zilizotokea wakati wa mazishi ya Sandra Nyongesa.

Marehemu ni mkewe diwani maalum wa zamani wa chama cha Ford-Kenya, Bw Philip Nyongesa, ambaye ni mpwawe Bw Wetang’ula.

Makachero walisema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya uchunguzi unaoendelea kuhusu ghasia zilizotokea katika mazishi hayo, baina ya vijana wanaomuunga mkono Bw Wetang’ula na Gavana Natembeya.

Bw Natembeya amekuwa akimkosoa Bw Wetang’ula kwa madai ya kutumia jamii ya Mulembe kujifaidi kisiasa, hali ambayo imezua uhusiano mbaya baina ya viongozi hao wawli.

Mkuu wa idara ya DCI katika kaunti hiyo, Bw Francis Kihara, hakuzungumzia lolote kuhusu kisa hicho, ijapokuwa alionya kuwa wale watakaopatikana na hatia watafunguliwa mashtaka.

“Huu ni mchakato wa kawaida. Tutakabiliana vikali na wale wanaoendeleza ghasia za kisiasa katika kaunti,” akasema Bw Kihara kwenye mahojiano na Taifa Leo.

Kwa muda mrefu yamekuwepo makabiliano makali ya ubabe wa kisiasa baina ya viongozi wa vyama vya Democratic Party of Kenya (DAP-K) na Ford-Kenya katika Kaunti hiyo ya Trans Nzoia.

Madiwani wanaomuunga mkono Gavana Natembeya katika kaunti hiyo, wamekuwa wakidai kwamba kuna njama zinazoendeshwa na uongozi wa Ford-Kenya kuhujumu serikali ya gavana huyo.

Pia wakati wa mazishi ya mzee wa jamii ya Abaluhya, Ruben Masengeli, katika kijiji cha Bidii, eneobunge la Kwanza, viongozi walizomeana hadharani kuhusu tofauti za kisiasa zinazoendelea kutokoka baina ya gavana Natembeya na Spika Wetang’ula.

Cheche kali baina ya viongozi hao zilianza wakati diwani wa zamani wa wadi ya Kapomoi, Ben Wanjala, aliye mshirika wa karibu wa Bw Wetang’ula, aliwalaumu viongozi wa DAP-K Kwa kumdharau kiongozi huyo.

Alimwonya Bw Natembeya kwamba atapigiwa kura kwenye uchaguzi wa 2027 kulingana na utendakazi wake.

“Haijalishi utatuhangaisha kwa kiwango kipi. Utapigiwa kura kulingana na vitendo vyako ifikapo mwaka 2027,” akasema Bw Wanjala, kwenye kauli aliyomwelekeza Bw Natembeya.

Lakini wakati akitoa kauli hiyo, alizomewa na baadhi ya waombolezaji.

Mbunge wa Kwanza, Ferdinard Wanyonyi, pia aliukosoa uongozi wa DAP-K kwa madai ya kuwakosea heshima viongozi wa Ford-Kenya katika eneo hilo.

“Hebu tuheshimu Ford-Kenya kama chama cha pili kilichodumu miaka mingi zaidi nchini. Hivi ndivyo demokrasia inahitaji,” akasema Bw Wanyonyi.

Hata hivyo, madiwani, wakiongozwa na Naibu Spika wa Bunge la Trans Nzoia Obed Mwale, waliukosoa uongozi wa Ford-Kenya kwa kudai viongozi wa chama hicho wanasuka njama za kumhujumu Bw Natembeya. Alisema wako tayari kukabili njama hizo.

“Kama bunge, tumeapa kushiriana na gavana ili kuharakisha maendeleo. Tuko tayari kumtetea dhidi ya wale wanaolenga kuhujumu uongozi wake,” akasema Bw Mwale.

Mratibu wa mikakati katika DAP-K Joshua Werunga, alidai kuna njama za wandani wa Bw Wetang’ula kumhangaisha Bw Natembeya na baadaye kumlaumu kwa kutotekeleza maendeleo kikamilifu.

  • Tags

You can share this post!

Habida Moloney: Nilitumia Sh500,000 kwa tiba ya koo...

Kituo cha Turkwel Gorge chapoteza mvuto, uvundo ukisheheni

T L