Mwanawe Ruto afuata nyayo za babake siasani
Na JUSTUS OCHIENG
IMEIBUKA kuwa huenda mwanawe Naibu Rais William Ruto, Nick Ruto, anajitayarisha kujitosa kwenye ulingo wa siasa nchini.
Na ijapokuwa hajatangaza rasmi nia yake kutaka kufuata nyayo za babake, amekuwa akishiriki kwenye shughuli mbalimbali zinazoashiria kuwa anajitayarisha kuwania wadhifa wa kisiasa.
Duru zinaeleza kuwa Nick anajitayarisha kuwania ubunge katika eneo la Turbo au huenda anaandaa mikakati ya mapema kumfanyia kampeni babake kwenye kinyang’anyiro cha urais mnamo 2022.
Taifa Leo imebaini kwamba kama babake, Nick, washirika wake wa karibu na vijana katika Chama cha Jubilee (JP) wameigawanya nchi katika maeneo kadhaa, ili kuyafikia makanisa na makundi ya vijana.
Dkt Ruto pia ameigawanya nchi kwenye makundi matatu, mkakati unaoonekana kama mipango ya mapema kwenye kampeni yake.
Kama babake, Nick anasema kuwa mpango wake unalenga “kuisaidia jamii.”
Bw Victor Ayugi, ambaye ni mmoja wa washirika wa karibu wa Nick na mwanachama wa kundi la Jubilee Youth League, ameeleza jinsi watazuru sehemu mbalimbali nchini.
Kwenye mahojiano, alisema kuwa shughuli zao zitajumuisha “kushiriki kwenye hafla za kuchanga pesa kuyasaidia makanisa na vijana ili kuwasaidia.”
“Hili hata hivyo halimaanishi kuwa tunajihusisha kwenye siasa. Hili halihusiani kwa vyovyote vile na siasa za 2022,” akasema Bw Ayugi.
Mnamo Jumapili, Nick aliandamana na vijana wengine wakiwemo Bw Ayugi, George Maina, Brian kati ya wengine, ambapo walishiriki kwenye hafla ya kuchangisha pesa katika Kanisa la Katoliki la Nyamasore katika Kaunti ya Siaya.
Kanisa hilo limo katika eneobunge la Rarieda, anakotoka Katibu Mkuu wa Jubilee Bw Raphael Tuju. Alihudumu kama mbunge wa eneo hilo kati ya mwaka 2002 na 2007.
Akihutubu kwenye hafla hiyo, Nick hakuzungumzia lolote kuhusu siasa.
Badala yake, aliwashauri wazazi kuhusu umuhimu wa kuwalelea watoto wao kanisani.
Alisaidia kuchangisha Sh800,000 huku akitoa mchango wake binafsi wa Sh250,000.
“Ili watoto wawe wenye maadili mema katika jamii, kuna haja ya kuwahamasisha kuhusu umuhimu wa kwenda kanisani. Kwa sasa, kuna changamoto nyingi zinazowakumba vijana, ambapo wanaweza kuziepuka tu kwa kumwogopa Mungu,” akasema.
Atoa ahadi
Aliahidi kuendelea kuyasaidia makanisa na vijana kote nchini, ili kuimarisha hali ya maisha ya vijana.
Bw Ayugi alisema kuwa baada ya hafla hiyo, wangeelekea katika Kaunti ya Nairobi kwa mchango mwingine, huku akiahidi kuzuru katika Kaunti ya Migori baadaye.
“Sisi hatujihusishi kwenye siasa lakini tunajaribu kuisaidia jamii,” akasema.
Duru zilieleza kuwa huenda Nick anajaribu kumfanyia babake kampeni katika eneo la Nyanza, hasa akiwalenga vijana.
Dkt Ruto amezuru eneo hilo mara moja pekee tangu uchaguzi wa 2017. Hata hivyo, amezuru maeneo ya Kisii na Kuria mara kadhaa.
“Nick anaonekana kufaa zaidi kuwafikia vijana katika eneo la Nyanza kwani bado hajajihusisha sana kwenye siasa,” akasema mmoja wa washirika wake wakuu ambaye hakutaka kutajwa.