Siasa

Niko tayari kwa EACC kunipiga darubini – Joho

September 30th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na WINNIE ATIENO

GAVANA wa Mombasa, Bw Hassan Joho, amesema yuko tayari kuchunguzwa kuhusu jinsi serikali yake ilivyotumia fedha za kukabiliana na janga la corona.

Baadhi ya madiwani katika Kaunti ya Mombasa wamekuwa wakimshtumu kwa ufujaji wa fedha za umma tangu achaguliwe kuwa gavana na tayari waliwasilisha malalamishi yao kwa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC).

Lakini Bw Joho alisisitiza kuwa yuko tayari kwa uchunguzi wowote huku akiwataka viongozi wote wa kisiasa kuwajibika.

“Ni muhimu kwa viongozi kukubali kukosolewa, kuchunguzwa na kuwajibika. Ni wajibu wetu kama viongozi kusikiza watu tunaowaongoza,” akasema.

Akiongea kwenye uzinduzi wa utafiti uliofanywa na shirika la kutetea haki za kibinadamu la Haki Africa kuhusu matumizi ya fedha za kupambana na Covid-19, Gavana huyo alisema ataendelea kukubali kukosolewa.

“Tunafaa tukubali kukosolewa na kushauriwa. Najua tutatofautiana lakini ni lazima viongozi wachunguzwe. Turuhusu mashirika ya kijamii kutusaidia katika kukabiliana na changamoto zinazotukabili,” alisisitiza.

Alionya kuwa viongozi wanaokataa kukaguliwa na mashirika ya kijamii au vyombo vya serikali hujuta baadaye.“Leo uko uongozini lakini kesho utaondoka na utaona uovu, uchafu na ufisadi ilhali hutakuwa na nafasi au uwezo wa kuchukua hatua yoyote kwa sababu uliruhusu vitendo sawa na hivyo,” akasema.

Kulingana na ripoti hiyo ambayo haijatolewa wazi kwa umma, serikali ya kaunti ya Mombasa ilitumia fedha kwa njia ifaayo.

Katika kutayarisha vituo vya afya kwa ajili ya janga hilo, serikali hiyo ya Gavana Joho ilikuwa na alama ya asilimia 92. “Katika kutoa huduma, serikali ya kaunti ilikuwa na asilimia 73 huku kusaidia wakazi kukabiliana na njaa ikiwa na asilimia 72,” ripoti hiyo ilisema.

Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir alisema mashirika ya kijamii yanafaa kushirikiana na serikali za kaunti ili kuhakikisha matumizi bora ya fedha za umma na uwajibikaji.

Ingawa idadi ya maambukizi imekuwa ikipungua katika kaunti hiyo, Bw Joho alisema kuna wasiwasi kutokana na kuongezeka kwa maambukizi katika gereza la Shimo la Tewa na miongoni mwa madereva wa malori.

“Katika kaunti ya Mombasa, visa vya corona vimepungua maradufu chini ya asilimia tano. Hii inaashiria kuwa tunatimia kudhibiti janga hili. Lakini tunaendelea kurekodi visa vingi vya corona kwa madereva wa malori na inasikitisha kuwa hata gerezani, idadi inaongezeka,” alisema Bw Joho.

Hata hivyo, gavana huyo alisema serikali yake itasaidia idara ya magereza kukabiliana na janga hilo.Aliwaagiza maafisa wake wa afya kushirikiana na wale wa gerezani kukabiliana na changamoto hiyo ya dharura ili kupunguza maambukizi.

“Tuko tayari kusaidia idara ya maregeza ili kukabiliana na janga hilo. Lazima tuwalinde wafungwa wetu maregezani na tuhakikishe tunazingatia kanuni za afya ili tukomesha virusi hivyo gerezani,” alisisitiza.

Shimo la Tewa ndilo gereza kubwa zaidi eneo la Pwani lenye idadi kubwa ya wafungwa, wakiwemo waliohukumiwa nje ya ukanda huo.