Oburu afichua alihofia mgawanyiko ungetokea baada ya Raila kufariki
KIONGOZI wa chama cha ODM, Dkt Oburu Oginga, amefichua kuwa aliwahi kumuonya kaka yake mdogo marehemu Raila Odinga kuhusu hatari ya kuzuka kwa mzozo mkali katika familia kubwa ya Odinga iwapo hawangetatua masuala ya kifamilia ambayo yalihitaji kushughulikiwa.
Katika mahojiano na Taifa Leo Dijitali, Dkt Oginga alisema aliogopa kuwa masuala ambayo hayakutatuliwa, ikiwemo usimamizi wa mali ya familia, siku moja yangeweza kuivunja familia ambayo kwa miaka mingi walilinda kwa umoja na bidii.
Anasema mazungumzo hayo ya tahadhari alifanya na Odinga kwa simu siku chache tu kabla ya kifo chake nchini India mnamo Oktoba 15.
Walikubaliana kukutana Dubai Oktoba 19 kujadili suala hilo, lakini mkutano haukufanyika baada ya Raila kuaga dunia.
Kwa mujibu wa Dkt Oginga, alimwambia ndugu yake kuwa ingawa wao wawili wameishi kwa umoja na safari ndefu ya kisiasa, kizazi kijacho kinaweza kukosa mshikamano kama wao, hivyo suluhu ya kudumu kwa ugavi wa mali ilikuwa muhimu ili kuepusha vita vya baadaye.
Alimhimiza Raila “kumaliza jambo hilo mara moja,” kwa kuhakikisha kila ndugu anapata chake na hakukuwa na cha kusalia kuweza kuchochea mivutano.
Dkt Oginga alisema hofu yake kuu ilikuwa kutotabirika kwa maisha na uwezekano wa wao wawili kufariki kabla ya masuala hayo kukamilishwa.
“Maisha ya binadamu ni ya muda mfupi,” alimkumbusha Raila.
“Kitu kikitokea kwako au kwangu kabla hatujamaliza haya, hawa vijana sioni kama wataungana kama sisi.”Lakini kabla ya kuchukua hatua yoyote, mauti yakamkumba Odinga.
Mazishi ya haraka ndani ya saa 72 kama alivyoagiza yalizidisha hisia za majonzi nchini, huku mamilioni wakimiminika Nairobi, Kisumu na Bondo.
Hata hivyo, chini ya wingu hilo la maombolezo, nyufa za migogoro katika familia ya Odinga sasa zimeanza kuonekana.Wakati wa sherehe za ODM@20 Mombasa, bintiye Odinga, Winnie, alitoa madai makali kwamba kuna njama ya baadhi ya vigogo kuuza chama alichokianzisha baba yake.
Chanzo cha ndani ya familia kilidokeza kuwa msimamo mkali wa Winnie unatokana na mvutano wa wiki kadhaa katika familia.
Tukio la kwanza lililodhihirisha mvutano huo ni kutohudhuria kwake hafla ya kumtawaza kaka yake Raila Junior kuwa msemaji wa familia.
Mzozo huo ulijitokeza kikamilifu wakati wa hafla ya miaka 20 ya ODM katika Mama Ngina Waterfront, MombasaKiini cha tofauti hizo ni nafasi ya ODM katika serikali jumuishi mpango ambao marehemu Odinga aliunga mkono kabla ya kufariki.
Winnie anaona mpango huo ukisimamiwa vibaya, huku Dkt Oginga akisisitiza ulikuwa msimamo wa mwisho wa Odinga.
Akiongea hadharani, Winnie alikosoa uongozi wa sasa wa ODM kwa ukali, akihoji uwezo wao wa kuendeleza “mpango mgumu” ambao zamani ulihitaji ujuzi wa Baba.Alitaka kuitishwa kwa Mkutano Mkuu (NDC) ili wanachama waamue nani anafaa kusimamia uhusiano wa ODM na serikali.
Kauli zake zilipandisha joto kwa baadhi ya wafuasi, lakini pia zikasababisha hasira miongoni mwa maafisa wa chama waliotafsiri matamshi yake kama yakumvunjia heshima Dkt Oginga.
Kwa upande wake, Dkt Oginga alijibu kwa utulivu, akisisitiza kuwa yeye ni mwanzilishi wa ODM na kwamba alikuwa karibu sana na Raila kwa miaka yote ya uhai wake.Alimwambia Winnie kuwa suala la usimamizi wa uhusiano wa ODM na serikali jumuishi litajadiliwa na familia huko nyumbani.