ODM yafichua lengo la vikao vya ‘Linda Ground’
CHAMA cha ODM kimeanzisha kampeni kali ya kulinda ngome zake kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027.
Kampeni hiyo kwa jina ‘Linda Ground’, inayoongozwa na kinara wa ODM, Dkt Oburu Oginga inajumuisha misururu ya shughuli za kisiasa ikilenga kuimarisha ushawishi wa chama hicho katika maeneo ya Nyanza, Magharibi na Pwani.
Mnamo wikendi, chama hicho kilipeleka kampeni yake ya ‘Linda Ground’ katika uwanja wa Sameta, Kaunti ya Kisii, kilipowahimiza wakazi kumuunga kinara wa chama Dkt Oburu huku ODM ikidhamiria kupinga ushawishi wa Jubilee unaozidi kushika kasi eneo hilo ukiongozwa na Dkt Fred Matiang’i.
Kama sehemu ya kampeni hiyo, ODM imetangaza mchakato wa kusajili wapigakura wapya 700,000 katika kaunti nne za Nyanza; Kisumu, Siaya, Homa Bay na Migori. Kaunti hizo nne kwa sasa zina jumla ya wapigakura waliosajiliwa milioni 2.2 kulingana na takwimu za Tume ya Uchaguzi (IEBC).
Mjini Kisii, Dkt Oburu alikiri kuwa ni kibarua kigumu kumrithi kisiasa marehemu kaka yake Raila Odinga ambaye aliongoza chama hicho kwa miaka 20.
“Baadhi ya watu wanasema viatu vya Raila ni vikubwa mno kwangu. Japo najua ni vikubwa, ninavijaribu. Siwezi kusalimu amri,” alisema Dkt Oburu, akisisitiza kupoteza chama hicho kutakuwa kuangusha historia ya kaka yake na Wakenya wanaotegemea ODM kufichua ukiukaji wa haki.
Wandani wa chama hicho wanaamini kudumisha ngome za jadi ni muhimu kwa ODM kutwaa sehemu muhimu katika serikali ijayo.
Aidha, chama hicho kimeashiria mipango ya kufanya mkataba kuhusu muungano kabla ya chaguzi na chama cha Rais William Ruto, UDA kwa dhamira ya kuunga mkono azma yake kuchaguliwa tena.
ODM imetangaza upya mamlaka yake kisiasa huku kukiwa na wasiwasi kuwa kutwaliwa na Rais Ruto huenda kukadidimiza chama hicho kabla ya 2027.
Mikakati ya chama hicho inalenga kudumisha viti vya bunge, bunge la kaunti na ugavana na hata kuvishinda vingine kwenye ngome za wapinzani.
Dkt Oburu tayari ameendesha mikutano ya hadhara katika maeneo ya Kibra, Nairobi, Busia, Kakamega na Kisumu, huku naibu kinara wa chama, Gavana Simba Arati akiendesha mkutano mkubwa wa kisiasamjini Kisii.
Muafaka baina ya ODM na UDA unapendekeza Sh450 bilioni kama mgao wa mapato kwa kaunti huku bajeti ya sasa ikitenga Sh415 bilioni, kiasi kilichoongezwa kutoka Sh380 bilioni katika bajeti ya 2024/25.