ODM yajikuta ikitokwa na jasho Kaspul bila Raila
CHAMA cha Orange Democratic Movement (ODM) kimejikuta katika mapambano makali ya kisiasa katika eneo bunge la Kasipul, ambalo kwa miaka mingi limekuwa mojawapo ya ngome zake thabiti.
Kampeni za uchaguzi mdogo wa Alhamisi zilipokamilika Jumatatu, ushindani mkali ulionekana kati ya mgombeaji wa ODM Boyd Were na mgombeaji huru Philip Aroko.
ODM imelaumu chama cha United Democratic Alliance (UDA), kinachoshirikiana nacho katika serikali jumuishi, kwa kufanya kampeni dhidi ya mgombea wake, jambo linalotishia kufichua udhaifu wa chama hicho bila mwongozo wa kinara wake wa muda mrefu, Raila Odinga.
Bw Aroko amefanya kampeni kali na amekuwa tishio halisi kwa ODM huku wakazi wengi wakihisi ushindi unaweza kuelekea upande wowote kati ya Were na Aroko, licha ya uchaguzi kuvutia wagombea 10.
Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga aliongoza kampeni za ODM, akishirikiana na viongozi wakuu wa chama hicho na kutumia rasilmali nyingi. Hata hivyo, hali si shwari kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Kauli kali ya Mbunge wa Homa Bay Town Peter Kaluma mwishoni mwa wiki imeonyesha kiwango cha tishio inayokumba chama hicho.
Bw Kaluma aliwashutumu magavana wa zamani Evans Kidero na Okoth Obado wanaohusishwa na UDA kwa kumpigia debe Aroko. Pia alimtaja Odoyo Owiti, mwandani wa UDA katika kaunti hiyo.
“Hatuwezi kuwa ndani ya serikali moja jumuishi halafu wanachama wa UDA wanampinga mgombeaji wetu. Rais anapaswa kuwadhibiti watu hawa,” Kaluma alisema.
Wakosoaji wanailaumu ODM kwa mchakato dhaifu wa uteuzi uliofanya baadhi ya wagombeaji kuamua kivyao wakiwa huru.
Inadaiwa kuwa viongozi wa juu walimpendekeza Were kabla ya chama kufanya uteuzi wake rasmi. Boyd analenga kuendeleza urithi wa babake, marehemu Ong’ondo Were.
“ODM haina mgombeaji Kasipul. Aliyevalishwa rangi za ODM ni mgombeaji binafsi wa Gladys Wanga. Kama wangehitaji ushirikiano wetu, wangefanya uteuzi wa haki,” alisema Odoyo.
Aidha alidai ODM haijawahi kuwakumbatia wanachama wa UDA tangu kuanza kwa serikali jumuishi. Alitaja tukio ambapo wafuasi wa UDA walidaiwa kufurushwa kutoka hafla ya wanawake Kasipul iliyohudhuriwa na Naibu Rais na Katibu wa Wizara ya Usalama wa Ndani.
Wachambuzi wanasema kutokuwepo kwa Raila Odinga katika kampeni za eneo hilo kumedhoofisha ushawishi wa ODM. Raila alikuwa na uwezo mkubwa wa kuwapigia debe wagombeaji wa chama, hususan kupitia ishara yake maarufu ya kuinua mikono ya wagombeaji.
Zaidi ya hayo, migawanyiko kati ya Gavana Wanga na Naibu wake Oyugi Magwanga imeendeleza mpasuko ndani ya chama.
Ijumaa, akiwa Wire, West Kamagak, Magwanga alikashifu mchakato wa uteuzi uliompendekeza Boyd Were, akisema haukuwa wa haki.
“Hakuna sheria inayosema ukifa, ni mwanao anapaswa kukurithi. Nimeambiwa nimuunge mkono Boyd lakini sitafanya hivyo,” Magwanga akasema.
Alieleza kutamaushwa na visa vya vurugu vilivyoshuhudiwa wakati wa uteuzi, ikiwemo uharibifu wa mali katika hospitali ya kibinafsi.
Tunapoelekea uchaguzi mdogo, Magwanga alisisitiza kuwa zoezi linapaswa kuwa huru na la haki na kwamba hakuna mtu anayepaswa kuingilia mchakato huo.