ODM yawaomba wanaomezea mate kito cha Msambweni kuwasilisha maombi
Na CHARLES WASONGA
KINYANG’ANYIRO cha kiti cha Msambweni kimeanza baada ya chama cha ODM kuwataka wagombeaji kuwasilisha maombi rasmi ya kutaka kuwania kiti hicho kwa tiketi ya chama hicho.
Kwenye ilani iliyotolewa Jumamosi Mwenyekiti wa Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi (NEB) katika ODM Cathrine Mumma awataka wale wanaotaka kugombea kiti hicho na viti vingine vinne vya udiwani kuwasilisha maombi yao mnamo Jumatatu Septemba 21, 2020.
“NEB inatoa notisi kwa wale wote wanaotaka kuwania kiti cha ubunge cha Msambweni na maeneo mengine wakilishi ya udiwani kuwasilisha maombi yao, katika fomu rasmi, katika makao makuu ya chama jumba la Chungwa kufikia Jumatatu jioni Septemba 21,” mwenyekiti huyo akasema kwenye taarifa.
Kuna wagombeaji watano ambao wamejitokeza ambao wametangaza nia ya kugombea kiti hicho kwa tiketi ya chama chama katika uchaguzi mdogo Desemba 15, 2020.
Wao ni; aliyekuwa diwani wa wadi ya Bongwe/Gombato Omar Boga, mwenyekiti wa ODM tawi la Kwale Nicholas Zani, Feisal Bader, Ali Mwakulonda na Sharlet Akinyi.
Kiti hicho kilisalia wazi mnamo Machi 9, 2020 kufuatia kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wa Muungano wa Wabunge wa Pwani (CPC) Suleiman Dori.
Chama cha ODM pia kitarajia kudhamini wagombeaji katika chaguzi ndogo za udiwani katika. Bw Feisal Bader anatoka katika ukoo moja na marehemu Dori.
Kando na Msambweni ODM pia inatarajiwa kuwadhamini wagombea katika chaguzi za udiwani katika wadi za Dobaso katika kaunti ya Kilifi, wadi ya Kisumu Kaskazini, (Kaunti ya Kisumu), wadi ya Kahawa Wendani (Kaunti ya Kiambu) na wadi ya Wundanyi/Mbale (Kaunti ya Taita Taveta).
Uchaguzi mdogo wa wadi ya Dobaso iliyoko eneo bunge la Malindi umeratibiwa kufanyika mnamo Aprili 28, 2021.
Tume huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilichelewesha chaguzi hizo kutokana na mlipuko wa janga la Covid-19 nchini mnamo Machi 13, 2020.