Peter Kenneth: Mlima Kenya wajua kujilinda dhidi ya siasa hasi
NA MWANGI MUIRURI
ALIYEKUWA mwaniaji wa urais mwaka wa 2013 Bw Peter Kenneth, amesema kwamba siasa hasi zinazojitokeza dhidi ya Mlima Kenya si geni, ni za tangu jadi.
Bw Kenneth ameonya kwamba siasa za aina hiyo ndizo zimeumba eneo la Mlima Kenya na kulipa umaarufu ambao hurejelewa na wachambuzi.
Kwenye mahojiano na Taifa Leo kwa njia ya kipekee, Bw Kenneth alisema kwamba hata siasa ambazo kwa sasa zimelipuka na kuangazia eneo hilo kama lililo kwa misukosuko, “si hoja kwani mambo yatatulia tu kwa wakati wake”.
Alisema kwamba hata vita vya viongozi vya ndani kwa ndani vikekuwepo tangu Kenya ijipe uhuru na ni vya kawaida watu wakibishania nafasi katika siasa na pia matarajio ya kesho.
Bw Kenneth alisema kila mara eneo hilo huwa na misukosuko ya udalali wa kisiasa na huwa inachochewa na wenyeji wakiunda mirengo ya kumenyana na hivyo basi kuunda nafasi za riziki, wengi wakisajiliwa kutetea au kupinga.
“Eneo hili limekuwa la kivumbi tangu jadi. Ni eneo ambalo lilikuwa jukwaa la dhuluma za mbeberu akitwaa mashamba na kuwakalia wenyeji kimabavu. Kisha tukaingia miaka 24 ya utawala wa Rais Daniel Moi (1978-2002) na pia tukavamiwa na genge la Mungiki kando na ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007/8,” akasema Bw Kenneth.
Mwanasiasa huyo ambaye aliwahi kuwa mbunge wa Gatanga pia aliongeza kwamba hakuna uchaguzi wowote wa kitaifa ambao Mlima Kenya haukuwa na mwakilishi “na katika hali hizo zote, eneo hili lilibakia limesimama”.
Aliongeza kwamba wenyeji wa Mlima Kenya ni watu wa bidii na huvunja migongo wakikimbizana na riziki.
“Sisi ndio hujipata pambaya zaidi uchumi ukizoroteka na kwa sasa ushuru wa juu wa serikali ya Rais William Ruto unatusinya si haba,” akasema.
Bw Kenneth alisema kwamba “eneo la Mlima Kenya huungana wakati kuna hatari inayoeleweka”.
Alisema kwamba licha ya kugawanyika kwa maeneo ya milima ya eneo hilo baada ya kutokea kwa msitu, ili kupokea bendera ya uhuru waliungana kumhifadhi Rais wa kwanza Hayati Mzee Jomo Kenyatta kuanzia 1963 hadi 1978.
Bw Kenneth aliongeza kwamba wenyeji hao waliingia kwa serikali ya Rais Moi, ambaye kwa sasa ni marehemu, wakiwa wameungana kwamba alikuwa hafai.
“Ndipo waliungana katika harakati za kupambania mfumo wa vyama vingi vya kisiasa licha ya kuwa na mirengo pinzani ndani yao ikiongozwa na Stanley Matiba na Mwai Kibaki (Rais wa Tatu wa Kenya) na pia wengine kandokando,” akasema.
Bw Kenneth alifafanua kwamba hata wakati wa referenda ya 2005 eneo hilo liligawanyika, Rais Kibaki akiwa kwa mrengo wa kuunga huku naye Uhuru Kenyatta akiwa wa kupinga.
“Hata Kibaki akiwa Rais alipingwa na akatukanwa na wengine. Uhuru Kenyatta pia alikumbana na upinzani wa ndani kwa ndani. Yaani kupingana hapa Mlima Kenya ni kawaida lakini dakika ya mwisho, tutaungana watu wakose kuamini,” akasema.
Alisema kwamba kwa sasa Bw Gachagua atapingwa, apigwe mnada na pia apewe masharti lakini “uthabiti na umoja wa malengo yetu utabakia imara”.
Bw Kenneth alisema ari kuu ya Mlima ni kuona utawala wa kuunganisha Wakenya ndio wawe na amani na ustawi.
“Aidha, ni vyema ieleweke kwamba Mlima huwa na chuki na utawala mbaya, kandamizi likija suala la ushuru, na unaoonyesha dharau na usaliti,” akasema.