Raila agonganisha seneti na wabunge
KATIKA jitihada zake za kutaka kudumisha rekodi yake kama mtetezi sugu wa ugatuzi, kiongozi la ODM Raila Odinga anaonekana kuendelea kuchochea zaidi vita vya ubabe kati ya Bunge la Kitaifa na Seneti na hivyo kuathiri utendakazi wa mabunge hayo.
Wiki hii, Bw Odinga alionekana kuwakera wabunge zaidi kwani mbali na kuendelea kampeni ya kutaka Hazina ya Ustawi wa Maeneo Bunge (NG-CDF) ipokonywe wabunge na kuwekwa chini ya usimamazi wa serikali za kaunti, sasa anapendekeza Seneti ipewe mamlaka zaidi.
Wadadisi wanaonya kwamba pendekezo kama hilo linapasa kutoka kwa raia wala si Bw Odinga au maseneta ili lisije likaonekana kuendeleza masilahi finyu ya wanasiasa hao.
Akiongea Jumatano baada ya kufanya mkutano wa faragha na maseneta katika majengo ya bunge, Bw Odinga aliunga mkono pendekezo la maseneta kwamba Katiba ifanyiwe marekebisho ili kuipa Seneti mamlaka ya kupitisha miswada inayohusu masuala ya fedha na usalama.
Ilivyo sasa, Bunge la Kitaifa ndilo lenye usemi mkubwa katika masuala ya utayarishaji na upitishaji wa bajeti ya kitaifa na miswada wa fedha inaosheheni mapendekezo ya kufadhili wa bajeti hiyo.
“Seneti ya Kenya inafaa kuwa na mamlaka ya juu kama ile ya Amerika, inayotekeleza mfumo wa utawala sawa na ule unaotelezwa nchini.
Kwa hivyo, Seneti ya Kenya inafaa kuwa na mamlaka zaidi si tu katika kuendeleza ugatuzi bali iwe na usemi wa mwisho katika masuala makuu ya uongozi,” Bw Odinga akaeleza.
Maseneta wamebuni wazo la kuanzisha mchakato sambamba wa marekebisho ya Katiba unaolenga kuwapa mamlaka zaidi katika masuala ya uongozi wa nchi.
Wamebuni kamati maalum itakayoongozwa na Kiongozi wa Wengi Aaron Cheruiyot na Kiongozi wa Wachache Stewart Madzayo kutayarisha mswada huo wa marekebisho ya Katiba.
Kamati hiyo inashirikisha maseneta wanasheria kama vile Mawakili Wakuu Tom Ojienda (Seneta wa Kisumu), Okong’o Omogeni (Nyamira) na maseneta Hillary Sigei (Bomet), Edwin Sifuna (Nairobi) na Catherine Mumma (seneta maalum).
Aidha, maseneta wamepinga Mswada wa Marekebisho ya Katiba, unaoungwa mkono na wabunge unaolenga kukita hazina ya NG-CDF kwenye Katiba.
Mtaalamu wa masuala ya kisheria na uongozi Barasa Nyukuri anashauri kwamba mchakato kama huu unapasa kushirikisha bunge la kitaifa na raia “ili upate uhalali”.
“Raila asionekane kuegemea upande mmoja wa maseneta. Mchakato wa marekebisho ya Katiba ni mzito na unapasa kuendeshwa kwa njia jumuishi, wananchi wakipewa usemi zaidi,” anaeleza.
Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi ameiambia safu hii kwamba wamekubaliana kukataa wazo la kubuniwa kwa Hazina ya Seneti kuhusu Uhakiki wa Utendakazi wa Serikali za Kaunti (SOF), itakayosimamiwa na maseneta kwani wabunge wanapania kutumia kupendekezo hilo “kuwahonga maseneta kupitisha mswada wa kuhalalisha NG-CDF.”
“Njia ya kipekee ya kuhalalisha NG-CDF ni kuwasilisha mswada katika kura ya maamuzi. Hii ni kwa sababu mswada huo unaenda kinyume na malengo ya katiba na muundo wa uongozi,” anasema Bw Osotsi.
Naye Seneta wa Kirinyaga James Murango aliunga mkono kauli ya Bw Osotsi akishikilia kuwa hazina ya NG-CDF inakiuka Katiba.“Aidha, tunataka Seneti ipewe mamlaka zaidi kama vile ya kupitisha Mswada wa Fedha na kuidhinisha Bajeti ya Kitaifa.
Hii ni kwa sababu masuala yote ya kifedha yanahusu kaunti,” Bw Murango akaeleza.Isitoshe, maseneta wanataka kuhusishwa katika mchakato wa kuwapiga msasa mawaziri, makatibu wa wizara, makamishna wateule wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) na watu wengine wanaopendekezwa kushikilia afisi kuu serikalini.