Raila akienda AUC Kenya itakosa upinzani wa nguvu – Mbunge
NA OSCAR KAKAI
HUKU viongozi wengi kutoka mirengo ya upinzani na serikali ya Kenya Kwanza wakiunga mkono azma ya kiongozi wa Azimio La Umoja-One Kenya Raila Odinga kuwa mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AU), Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Pokot Magharibi Rael Kasiwai amejitokeza kupinga hatua hiyo akisema kuwa italemaza upinzani nchini.
Kulingana na Bi Kasiwai ambaye alikuwa akihutubia wakazi wa eneo la Sigor mnamo Ijumaa, huenda upinzani ukakufa bila endapo Bw Odinga atakaa mbali kidogo na siasa za Kenya.
Aidha, Bi Kasiwai alisema kuwa kazi ya upinzani ni kuisukuma serikali na kuangalia mahali kuna utepetevu na Bw Odinga ndiye kiongozi ambaye yuko katika nafasi nzuri kuendelea na kazi hiyo.
“Bw Odinga yuko na uzoefu kwa kazi ya upinzani na kuondoka kwake huenda kukabuni mwanya ambapo serikali haitakuwa na mtu wa kuisukuma,” akasema Bi Kasiwai.
Aliongeza kuwa siasa za Kenya zitakosa mbabe wa kisiasa wa kuisukuma serikali ya Kenya Kwanza kutimiza ahadi ambazo ilitoa kwa Wakenya.
Ni kinaya kwa sababu mwakilishi huyo alionekana kuchukua mkondo tofauti na wa viongozi wa Kenya Kwanza.
Bi Kasiwai (Kenya Union Party-KUP) alisema kuwa pamoja na kinara wa chama chake Prof John Lonyangapuo, waliondoka kutoka mrengo wa Azimio na sasa wako kwa Kenya Kwanza.
“Tulikuwa tumepotea lakini sasa tuko nyuma ya Rais William Ruto na mwaka wa 2027 tutampea kura za kutosha. Kikosi ambacho mliona kwenye picha ya pamoja na Rais wakati wa mkutano mjini Naivasha juzi ndio tosha. Tulichaguliwa kwa chama cha KUP lakini sasa tuko ndani ya serikali ya Kenya Kwanza,” alisema.
Akiwa pamoja na mbunge wa Sigor Peter Lochakapong wa chama cha Rais – United Democratic Alliance (UDA), wawili hao walimhakikishia Rais Ruto uungwaji mkono kwenye uchaguzi mkuu ujao wa 2027 kutoka kwa wakazi wa eneo nzima la Pokot.
Kwa upande wake, Bw Lochakapong alisema kuwa uchumi wa nchi umeanza kuimarika na wanamuunga kwa dhati kiongozi wa nchi.
Bw Lochakapong aliwasuta baadhi ya viongozi wa eneo hilo ambao walikuwa kwenye upinzani na sasa wanataka kuingia serikalini kupitia njia za mkato huku akiwataja kuwa waongo na wasioaminika.
“Hawako pamoja nasi na hawako kwa serikali na yale wanawaeleza ni uongo na propaganda,” alisema Bw Lochakapong.
Tayari Rais Ruto na viongozi wengi ndani ya serikali wameonyesha nia ya wazi kumuunga mkono Bw Odinga kuwania uenyekiti AUC.
Mapema wiki hii Rais Ruto na Bw Odinga walikutana naye Rais wa Uganda Yoweri Museveni katika boma lake la mashinani la Kisozi hatua ambayo ilionekana ya kumtafutia Bw Odinga ungwaji mkono.
Ikiwa Bw Odinga atakuwa mwenyekiti wa AUC, basi atalazimika kuacha siasa za Kenya. Nafasi hiyo itakuwa wazi Januari 2025 baada ya kukamilika kwa kipindi cha pili cha mwenyekiti wa sasa Moussa Faki.
Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka yuko mbioni kutoshea kwa viatu vya Bw Odinga katika mrengo wa Azimio.