Siasa

Raila apangua mfumo wa usimamizi ODM kuzima blanda za uteuzi

January 11th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA CHARLES WASONGA

CHAMA cha Orange Democratic Movement (ODM) kimependekeza kuvunjilia mbali Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi (NEB) na kugatua majukumu yake hadi katika ngazi za kaunti katika kile kinachosemekana ni njia ya kumaliza udanganyifu nyakati za kura ya mchujo.

Hatua hiyo iliyotangazwa Jumatano baada ya mkutano wa Baraza Kuu la Usimamizi (CMC) ulioongozwa na Raila Odinga pia inalenga kuimarisha usimamizi wa shughuli na chaguzi za chama hicho na kuyapa matawi ya ODM usemi katika shughuli zake.

Nafasi ya NEB itachukuliwa na asasi mpya inayojulikana kama Kamati Shirikishi itakayosimamia chaguzi na mchujo wa ODM katika ngazi za kitaifa.

Kamati hiyo yenye wanachama watatu pia itatoa ‘mwelekeo’ kwa kamati za kusimamia chaguzi na kura za mchujo katika ngazi za kaunti.

Kamati hiyo Shirikishi itakuwa na wanachama watatu ambao watawajibika moja kwa moja kwa Kamati ya CMC.

“Kuanzia sasa, chaguzi zote za chama zitasimamiwa katika ngazi za Kaunti na Washirikishi Wawili wa Chaguzi, mwanamume mmoja na mwanamke mmoja watakaosimamia kila kaunti,” Katibu Mkuu wa ODM, Wakili Edwin Sifuna akasema baada ya kikao cha CMC.

Ili kudumisha utendakazi mzuri, ODM imeteua wanachama wawili wa NEC kuhudumu katika Kamati mpya Shirikishi katika ngazi ya Kitaifa.

Wao ni Emily Awita na Richard Tairo. Mwanachama wa tatu aliyependekezwa ni Beatrice Askul.

Bi Awita amependekezwa kuwa mwenyekiti wa Kamati hiyo Shirikishi ya Uchaguzi katika Ngazi za Kitaifa.

Bodi ya NEB ilikuwa inaongozwa na Seneta Maalum Catherine Mumma.