Siasa

Raila awaweka wazee kando akijiandaa 2022

July 17th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na BENSON MATHEKA

KIONGOZI wa ODM, Bw Raila Odinga, amesajili washauri vijana katika juhudi za kutia nguvu azma yake ya kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Kinyume na awali alipotegemea wandani wakongwe kutoka ngome yake ya siasa ya Nyanza, sasa ametandaza nyavu zake na kuwasajili viongozi barobaro kutoka jamii na maeneo mengine nchini.

“Bw Odinga amekumbatia washauri vijana kufuta dhana kwamba aliotegemea kwa muda mrefu walikuwa wakimpotosha kwa kuwa na misimamo mikali. Walikuwa pia wepesi wa kutoa siri kwa vyombo vya habari. Hii ndiyo sababu aliwaacha nje wakati wa mazungumzo yake na Rais Kenyatta hadi wakaafikia handisheki,” asema mdadisi wa siasa, Bw Thomas Maosa, ambaye pia ni wakili wa Mahakama Kuu.

Anasema Bw Odinga anamwamini sana Mbunge wa Suna Mashariki, Bw Junet Mohammed na Gavana wa Mombasa, Bw Hassan Joho, kwa sababu ya uaminifu wao kwake.

“Wawili hao wako na nguvu, pesa na hawatoki katika jamii yake. Wanaweka siri ilivyoshuhudiwa wakati Junet alipoficha kuhusu mazungumzo yaliyozaa handisheki,” alisema Bw Maosa.

Wiki jana, wawili hao walienda hadi Dubai kwa ndege ya kukodisha kumuona Bw Odinga hospitalini, hatua ambayo wadadisi wanasema inadhihirisha imani yake kwao.

Hii ilikuwa siku mbili baada ya Bw Junet kukutana na Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Taifa, Bw Amos Kimunya, kutatua mzozo kuhusu uanachama wa kamati tatu muhimu za bunge.

Ripoti zilisema ni Bw Odinga aliyemtuma Bw Junet kutatua mzozo huo, baada ya kiongozi wa wachache , Bw John Mbadi kutofautiana na Bw Kimunya.

Bw Junet alikuwa mwanasiasa wa pekee aliyeandamana na Bw Odinga kutangaza muafaka wake na Rais Kenyatta. Waliokuwa wandani wake wa miaka mingi hawakuwa na habari kuhusu mazungumzo hayo.

Bw Joho amenukuliwa akisema kwamba Bw Odinga alikuwa amemdokezea mipango ya kuridhiana na Rais Kenyatta.

Wakati Gavana Anne Waiguru alipokuwa kwenye hatari ya kutimuliwa, Bw Junet ndiye aliyetangaza kuwa kama ODM walikuwa wameamua kumuokoa.

Kabla ya handisheki, Bw Odinga alikuwa akitegemea zaidi ushauri wa wandani wake wa kisiasa kutoka Nyanza hasa Seneta James Orengo wa Siaya na Gavana wa Kisumu, Prof Anyang’ Nyong’o.

“Sidhani amewatupa Orengo na Nyong’o. Anawahitaji sana kwa ushauri wao hasa kuhusu sera. Alichofanya ni kubadilisha mbinu. Raila anahitaji tajriba yao pana katika siasa, sheria na utawala,” akaeleza Bw Maosa.

“Baba hawezi kumtupa Orengo japo kuna nguvu mpya za kujiandaa kwa uchaguzi wa mwaka wa 2022,” alisema mbunge mmoja wa ODM ambaye aliomba tusitaje jina lake kwa sababu za kibinafsi.

Kwa sasa Bw Orengo ndiye kiongozi wa wachache katika Seneti.

Mdadisi wa siasa, Bw Joseph Mbindyo anasema kwamba Bw Odinga anaunda kundi la washauri waaminifu na wanaoelewa umuhimu wa handisheki.

“Anapanua kundi la washauri kwa vipimo vya uaminifu, eneo na ushawishi wao akilenga 2022,” asema Bw Mbindyo.

Anasema kwa kuwakumbatia Bw Joho na Bw Junet, Bw Odinga analenga pia kura za eneo la Kaskazini Mashariki, licha ya kuwa amechaguliwa Nyanza.

“Wawili hao wana mapato, ujasiri, ushawishi na uaminifu unaowafanya kutegemewa na Bw Odinga,” akasema Bw Mbindyo.