Siasa

Raila hapumui: AU yafungulia mlango wawaniaji zaidi wa kiti anachomezea mate Odinga

May 31st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA AGGREY MUTAMBO

MUUNGANO wa Afrika (AU) umefungua malango yake kwa wagombeaji zaidi katika uchaguzi ujao wa mwenyekiti na naibu wa Tume ya Bara (AUC) kuwasilisha nakala zao au kujiondoa na kuwaachia nafasi wapinzani wao.

Tarehe hizo mpya zinamaanisha wapinzani sharti wawasilishe kwa mataifa yao mtawalia stakabadhi zao za wasifu, taarifa ya maono na jinsi wanavyonuia kuangazia masuala ibuka katika bara hili.

Ni hatua ya kwanza kwa wagombezi kudhihirisha azma ya kuhudumu kama viongozi wa afisi kuu ya AU.

Wawaniaji wanne tayari wametangaza wazi kwamba watagombea.

Kiongozi wa Upinzani, Raila Odinga, Waziri wa Masuala ya Kigeni, Djibouti, Mahmoud Ali Youssouf, aliyekuwa waziri wa Masuala ya Kigeni Somalia, Fawzia Yusuf Adam na aliyekuwa naibu rais, Ushelisheli, Vincent Meriton, tayari wanaungwa mkono na mataifa yao.
Chini ya sheria za sasa za AU, kiti cha mwenyekiti wa AUC kitagombewa na mataifa yaliyo katika eneo la mashariki pekee huku wadhifa wa naibu ukiwaniwa na eneo la Afrika Kaskazini. Iwapo mgombezi mwanamume au mwanamke atashinda kuwa mwenyekiti, naibu atahitajika kuwa wa jinsia tofauti.

Kulingana na notisi ya uchaguzi iliyochapishwa wiki iliyopita, AU ilisema wawaniaji watawasilisha maombi kupitia mataifa yao.

Hata hivyo, wawaniaji watakaofika debeni watateuliwa baada ya mchakato mrefu. Watapigwa msasa na jopokazi la wataalam kabla ya uchaguzi huo utakaofanyika Februari 2025.

Nyadhifa zote za tume hiyo: mwenyekiti, naibu na makamishna sita ziko wazi kuwaniwa lakini kila eneo litapewa nyadhifa kulingana na kile ambacho viongozi wataafikiana kama vile “kanuni ya ujumuishaji kimaeneo” wenye haki.

Hii inamaanisha makamishna sita watatoka maeneo yaliyosalia ya kusini, kati na magharibi. “Kila eneo huamua mchakato wake binafsi wa kuteua wagombeaji kwa wadhifa ambao limefuzu,” inasema notisi.

Eneo kisha litawasilisha orodha yake kwa jopokazi la wataalam kufikia Agosti 6.

“Wagombea ambao majina yao yaliwasilishwa na eneo ndio pekee watakaoangaziwa katika mchakato wa uteuzi utakaotekelezwa na Jopokazi la Eminent Africans. Isitoshe, Mataifa Wanachama ambayo hayajawekewa vikwazo na AU ndiyo tu yatakayoruhusiwa kuwasilisha wagombea.”

Ina maana kwamba mataifa ambayo kwa sasa yamewekewa vikwazo kwa kushiriki mapinduzi ikiwemo Sudan, Gabon, Niger, Mali, Burkina Faso na Guinea hayajafuzu kuwania wadhifa wowote.