• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
Raila kuokoa jahazi makinda wake wa Azimio wakikwama

Raila kuokoa jahazi makinda wake wa Azimio wakikwama

NA WYCLIFFE NYABERI

KIONGOZI wa Wiper Kalonzo Musyoka, amesema Muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya utaendelea kukosoa utawala wa Kenya Kwanza kama kawaida hata ikiwa Raila Odinga anayesifika kwa kuchuna serikali sikio, atapata kiti cha Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).

Bw Musyoka alisema upinzani hautabaki kigae na kwamba ikitokea Rais William Ruto anawazidi nguvu na kufinya Wakenya, basi Azimio watatafuta usaidizi wa Bw Odinga hata angalau kwa wiki moja bila kujali ikiwa atakuwa mwenyekiti wa AUC au la.

Akizungumza Migori katika siku yake ya mwisho ya ziara yake ya siku tatu katika eneo la Nyanza Kusini, Bw Musyoka alisema Azimio itasalia imara katika kubainisha dhuluma serikalini.

“Kwa sababu Raila anaenda AU, hiyo si kusema kwamba sisi kama Wakenya tutanyamaza tunapokanyagwa. Wakitulemea zaidi tunaweza kumuambia Bw Odinga ‘njoo hata wiki moja tusaidiane hawa watu wanatulemea’. Au vipi?” Bw Musyoka akasema katika mji wa Awendo.

Alimpongeza Waziri Mkuu huyo wa zamani kwa uamuzi wake wa kuwania nafasi hiyo ya bara na kumtakia kila la heri.

“Tumezungumza kwa kirefu na Bw Odinga. Unajua tumetoka naye mbali sana lakini siwezi kuwaambia. Mkiniona hapa jueni kuwa Bw Odinga mwenyewe yuko hapa. Tumetoka mbali. Tunataka kuacha tabia ya kuiba kura. Kama kura yake isingeibwa, angemaliza muhula wake tangu 2013,” Bw Musyoka aliongeza.

Alisema Bw Odinga bado ana kazi ya kufanya kwa ajili ya nchi hii kwa sababu ilikubaliwa katika Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo (Nadco) kwamba lazima ashiriki katika uundaji wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) pamoja na rais Ruto.

“Ndio maana tunasema katika tume ijayo ya uchaguzi, tumekubaliana katika Nadco kwamba lazima tume iundwe kati ya Rais Ruto na Bw Odinga,” makamu huyo wa zamani wa rais alisema.

Katika mji wa Migori, kiongozi wa Democratic Action Party of Kenya (DAP-K) Eugene Wamalwa alisema Kenya itaweka historia kama nchi ya kwanza ya Afrika Mashariki kutoa mwenyekiti wa AUC.

“Leo tunataka kuwaambia watu wa Migori na Nyanza kwamba watu wengi wamekuwa na hofu kwamba Baba akienda itakuwaje? Nataka kuwaambia leo kwamba msiogope. Mioyo yenu isifadhaike kwa kuwa tunajua jinsi Baba amekuwa akitaka kuwa Rais wa Kenya,” Bw Wamalwa alisema.

Aliendelea kwamba kupitia Raila Amollo Odinga, watu wa Nyanza wataweka historia tena.

“Mtaleta mwenyekiti wa kwanza wa AUC kutoka Afrika Mashariki,” Bw Wamalwa aliongeza.

 [email protected]

  • Tags

You can share this post!

Kalonzo aishambulia serikali kwa kukandamiza uhuru wa...

‘Singo mothers’ sasa wakimbilia Fida kutafuta sapoti ya...

T L