Raila: Mwindaji anayejua kujitafutia windo chakani
NA WANDERI KAMAU
KIONGOZI wa Azimio la Umoja Raila Odinga, ameibukia kuwa mwanasiasa anayejua kujijenga upya na kutorokea baridi ya kisiasa, hata wakati anaposhindwa kwenye chaguzi za urais.
Tangu alipowania urais kwa mara ya kwanza mnamo 1997, Bw Odinga amebuni mbinu ya kutumia ujanja wa kisiasa kuhakikisha “anafaidika” pia kutoka kwa serikali inayochukua uongozi.
Kulingana na wadadisi wa siasa, hilo limedhihirishwa na juhudi zinazoendeshwa na Rais William Ruto kumpigia debe Bw Odinga kupata uungwaji mkono wa mataifa mengine barani Afrika, kwenye nia yake ya kuwania uenyekiti katika Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).
Kinaya ni kwamba, licha ya Rais Ruto kuendesha juhudi hizo, wawili hao walikuwa washindani wakali kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022, kiasi kwamba walikuwa wakielekezeana cheche kali za maneno wakati wa kampeni.
Baada ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kumtangaza Dkt Ruto kama mshindi wa uchaguzi wa urais, Bw Odinga na washirika wake katika Azimio waliapa kutomtambua Dkt Ruto kama Rais.
Hata hivyo, wawili hao baadaye waliondoa tofauti zao, duru zikieleza tayari kuna handisheki fiche baina ya vigogo hao wawili.
Wadadisi wanasema Rais Ruto na Bw Odinga walibuni handisheki hiyo kwenye kikao cha faragha kilichofanyika Oktoba mwaka uliopita jijini Mombasa.
Kikao hicho kilimshirikisha rais wa zamani wa Nigeria, Bw Olusegun Obasanjo.
“Hatua ya Rais Ruto kuanza kumfanyia kampeni Bw Odinga kuwania nafasi ya mwenyekiti katika AUC, inamsawiri Bw Odinga kama mwanasiasa mjanja mwenye uwezo wa kujiunda upya, kwa kuhakikisha kuwa pia amefaidika kutoka wa serikali iliyopo mamlakani,” asema Bw Micah Mutai, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.
Matukio mengine yanayotajwa kumsawiri Bw Odinga kama mwanasiasa mjanja ni hatua yake kubuni ushirikiano na Rais Mstaafu (marehemu) Daniel Moi, ambapo aliteuliwa kama Waziri wa Kawi mnamo 1998.
Wakati huo, Bw Odinga alibuni ushirikiano wa kisasa na Bw Moi, ambapo wawili hao waliunganisha vyama vya Kanu na National Development Party (NDP)—chake Bw Odinga—na kubuni New-Kanu.
Baada ya Bw Odinga kushindwa na Rais Mstaafu (marehemu) Mwai Kibaki kwenye uchaguzi wa urais wenye ushindani mkali wa 2007, alikataa kutambua matokeo hayo.
Msimamo mkali wa Bw Odinga ndio ulimfanya kuteuliwa kama Waziri Mkuu kati ya 2008 na 2013. Washirika wake wa karibu pia walifaidika kutokana na nyadhifa za mawaziri kwenye Serikali ya Muungano wa Kitaifa.
Baada ya uchaguzi mkuu wa 2017, Bw Odinga alianzisha maandamano makali dhidi ya Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta, huku akikataa kutambua ushindi wake.
Kama njia ya kutuliza hali, ilimlazimu Bw Kenyatta kubuni handisheki na Bw Odinga.
Wadadisi wanasema kuwa ikiwa Bw Odinga atashinda uenyekiti katika AUC, basi hilo litamsawiri kama mwanasiasa mjanja, anayejua “kuchumia kivulini”.