• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Refaranda: Wamalwa kupinga miswada ya kubuni vyeo

Refaranda: Wamalwa kupinga miswada ya kubuni vyeo

NA WANDERI KAMAU

ALIYEKUWA Waziri wa Ulinzi Eugene Wamalwa, amesema ataongoza kampeni za mrengo wa ‘La’ ikiwa kutakuwa na kura ya maoni kupigia kura miswada ya kuwatengenezea wanasiasa vyeo kama ilivyopendekezwa na Ripoti ya Kamati ya Mazungumzo ya Kitaifa (Nadco).

Kulingana na Kamati ya Pamoja ya Haki na Masuala ya Sheria katika Bunge la Kitaifa na Seneti (JLACS), itawalazimu Wakenya kushiriki kwenye kura ya maamuzi ili kupitisha ama kuangusha miswada ambayo itaathiri mfumo wa uongozi.

Miswada itakayowahitaji Wakenya kushiriki kwenye kura hiyo ni ule unaopendekeza kubuniwa kwa Afisi ya Kiongozi Rasmi wa Upinzani na ule unaopendekeza kuhalalishwa kwa Afisi ya Mkuu wa Mawaziri.

Lakini Jumanne, Bw Wamalwa, aliye pia kiongozi wa chama cha Democratic Action Party of Kenya (DAP-K), alisema kuwa atafanya hivyo kwani ripoti ya kamati hiyo haikungazia masuala yanayowahusu raia.

Kwenye mahojiano na kituo cha redio cha Inooro FM, Bw Wamalwa alisema kuwa baadhi ya masuala muhimu yaliyowasilishwa na mrengo wa Azimio, hasa kuhusu gharama ya juu ya maisha hayakujumuishwa kwenye ripoti hiyo.

Hivyo, alisema kwamba “hatawasaliti wananchi kwa kuungana na viongozi kutetea maslahi yao”.

“Bila shaka, kilicho wazi ni kuwa ripoti hii haukutilia maanani suala la kupanda kwa gharama ya maisha. Tunavyozungumza sasa, bei ya mafuta ingali juu. Mafuta ndiyo msingi wa kila kitu nchini. Ikiwa serikali haitapunguza bei ya mafuta zaidi, basi hatuwasaidii wananchi kwa vyovyote vile,” akasema Bw Wamalwa.

Kiongozi huyo alikanusha madai kwamba analenga kujijenga kisiasa kutokana na msimamo wake, ikizingatiwa kuwa ametangaza atawania urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2027.

“Tangu mwanzo, msimamo wangu umekuwa mmoja, kwamba lazima ripoti hiyo ingejumuisha mikakati ya kupunguza gharama ya maisha. Sijabadilisha kauli yangu hata kidogo. Ikiwa lengo langu lingekuwa kujijenga kisiasa, basi ningekuwa nikibadilisha misimamo yangu. Sijali hata ikiwa nitakuwa peke yangu katika safari hii,” akasema Bw Wamalwa.

Licha ya ripoti hiyo kuwasilishwa kwa Rais William Ruto na kiongozi wa Azimio la Umoja, Bw Raila Odinga, Bw Wamalwa alikataa kuitia saini, akiikosoa kwa “kutojumuisha masuala yanayowahusu raia”.

Kwenye utayarishi wa ripoti hiyo, mrengo wa Kenya Kwanza uliongozwa na Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wah huku ule wa Azimio ukiongozwa na kiongozi wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka.

  • Tags

You can share this post!

Polisi waamriwa kuvunja Mungiki katika steji ya Sagana

Muziki mtamu unahitaji msanii aliyeenda shule – Span One

T L