Rigathi apanga kumtafuta Uhuru na Ndindi Nyoro kumfungia nje Ruto Mlimani
ALIYEKUWA Naibu wa Rais Rigathi Gachagua amefichua kuwa amebuni mikakati mipya ya kumng’oa Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu wa 2027 akifafanua kuwa upinzani utatembelea kila eneo ili kuwaeleza wananchi mikakati hiyo.
Aidha, alikanusha vikali kauli ambayo imekuwa ikitolewa mara kwa mara na Rais Ruto kuwa upinzani hauna ajenda na mbinu ya kumbandua madarakani, akiapa kuwa watamwonyesha kivumbi debeni.
Bw Gachagua anapania kuzindua mipango minane mwaka huu ya kumsaidia kudhibiti kura za Mlima Kenya kuelekea 2027.
Utekelezaji wa baadhi ya mipango hiyo utaongozwa na Naibu Kiongozi wa DCP, Cleophas Malala.
“Baada ya mkutano na wabunge wanaounga maono yetu, nimeibua Mpango wa Kutekelezwa mwaka huu. Aidha, nimempa naibu wangu kibarua cha kuongoza utekelezaji huo kwa niaba ya chama cha DCP,” akasema Bw Gachagua.
Mojawapo ya mikakati mikuu ambayo wadau wa DCP wanapania kutekeleza kwa njia zote ni ushirikiano thabiti kati ya Bw Gachagua na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta na Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro.
Katika siku za hivi karibuni, Bw Gachagua na Nyoro wamemtetea Bw Kenyatta dhidi ya shutuma alizoelekezewa na baadhi ya wafuasi wa vyama vya UDA na ODM, ishara kwamba mipango ya wazee wa Agikuyu inaonyesha dalili za kufaulu.
Kuhusu mkakati wa pili, mbunge huyo wa zamani wa Mathira alisema, “Kila kitu kimekamilika. Tutazuru maeneo mbalimbali kuwaonyesha Wakenya mpangilio wetu wa maendeleo na mbinu za kumng’atua Ruto,” akasema Bw Gachagua alipohutubia vyombo vya habari mjini Kilifi wikendi.
Aliorodhesha usajili wa wapigakura na kukabiliana na jambo alilotaja kama uongo wa Rais Ruto kama mkakati wa tatu wa kupambana na utawala wake.
Hatua ya nne itakuwa kuwahimiza wapigakura wajitokeze kwa wingi kumwondoa Rais kupitia uchaguzi kisha mkakati wa tano utakuwa upinzani kulinda kura zake.
Mikakati miwili itakayosalia ni kukabiliana na Rais kupitia Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) na kortini baada ya kumbwaga uchaguzini halafu mwishowe waanze utawala wao.
Kuhusu madai kuwa kambi yake inaendelea kutorokwa na waliokuwa wandani wake, Bw Gachagua alisema hana wasiwasi kwa sababu jambo la muhimu ni kuwa na ufuasi wa wananchi wa kawaida.
“Rais Ruto ndiye anastahili kuingiwa na uoga hasa ikizingatiwa kuwa wanasiasa anaodai ni wandani wake, wanapanga kumhepa ili kujiunga na upinzani. Azma yake ya 2027 hivi karibuni itakuwa hatarini,” akaongeza.
Ni katika mahojiano hayo ambapo alikanusha kwamba Bw Malala amegura kambi yake akisema seneta huyo wa zamani wa Kakamega amelemewa na mafua.
“Mabloga wa Ruto ni watu wa ajabu na wale ambao wanaondoka DCP hawakuwa watu wetu.
“Iwapo wewe ni jasusi katika DCP ondoka kabla tukuondoe na wale wanaoondoka kwa sababu tumekataa ombi lao la kupewa tikiti moja kwa moja pia nao waende watakakopendelewa,” akasema.
Kauli hiyo inaonekana kumlenga Mbunge wa Juja George Koimburi ambaye alihama DCP wiki jana akidai Bw Gachagua anawatapeli wanasiasa hela kwa ahadi ya kupata tikiti ya chama hicho.
Hata hivyo, Bw Gachagua alisema kujiunga au kuondoka ndani ya chama cha kisiasa ni jambo la kawaida.
Kuhusu siasa za Pwani, kiongozi huyo alisema upinzani ulishaamua kumuunga mkono Mbunge wa Nyali Mohamed Ali awanie ugavana 2027.
“Tumekubaliana na Kalonzo kumuunga ila kile ambacho hatujakubaliana ni chama kipi atakachotumia 2027 kati ya Wiper na DCP,” akasema.
Alimrejelea Bw Ali ambaye amehudumu mihula miwili bungeni, kama kiongozi mchapakazi na asiyekuwa na doa la ufisadi.
Pia aliahidi kupambana na tatizo la matumizi ya mihadarati ambalo limekita mizizi eneo la Pwani kwa miaka mingi.
Alidai kuwa baadhi ya wanasiasa kutoka Pwani ni walanguzi wa dawa za kulevya ambao wamekuwa wakipiga vita juhudi za kutokomeza tatizo hilo kwa sababu wanahudumu serikalini.
“Tukiunda serikali walanguzi wa dawa za kulevya watafungwa na kuuza dawa hizo kutakuwa haramu nchini. Hospitali zote za Level Four zitakuwa na idara ya urekebishaji tabia,” akasema.