Siasa

Ruto ajionea ukaidi dhidi ya Gachagua ziarani Mlima Kenya

February 16th, 2024 3 min read

NA MWANGI MUIRURI

BAADHI ya wanasiasa wa Mlima Kenya wamejitokeza waziwazi kukaidi juhudi za Naibu Rais Rigathi Gachagua za kuwaunganisha, sasa ikibidi Rais William Ruto kuingilia kati na kutangaza kwamba atawaunganisha yeye mwenyewe.

Kauli hiyo ya Rais inaonekana kuwa ya kutoa tahadhari kwamba shida ya kisiasa iliyoko eneo la Mlima Kenya kwa sasa inahitaji jitihada za kiwango cha juu kuliko zile za Bw Gachagua.

Hii ni baada ya wanasiasa wa Kaunti ya Kiambu kulumbana hadharani mnamo Jumamosi wakati Rais Ruto alianza ziara ya siku tatu katika kaunti za Kiambu, Murang’a, na Kirinyaga kuzindua miradi ya maendeleo.

Katika Kaunti ndogo ya Lari ambapo Rais alihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara, viongozi wa Kiambu wakiongozwa na Gavana Kimani Wamatangi, mbunge wa Thika Alice Ng’ang’a, Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wah na wengine walikemeana hadharani kwa cheche za maneno zilizojaa hisia kali huku Rais Ruto na Bw Gachagua wakishuhudia.

Hii ni licha ya Bw Gachagua kuwa alikuwa ameandaa mkutano wa umoja katika Kaunti ya Murang’a akiwaleta pamoja wanasiasa 147 katika eneobunge la Kigumo Jumamosi na kutangaza kwamba “Rais sasa atazuru eneo ambalo nimeliunganisha, liko na ajenda ya kimaendeleo na  ambalo nitazidi kulileta pamoja ili kuongea kwa sauti moja”.

Wakati maji yalizidi unga, Rais Ruto alichukua fursa hiyo kutangaza kwamba “sasa mimi nitawaleta pamoja viongozi hawa ili tukubaliane nao jinsi ambavyo tunaweza kusonga mbele kwa umoja”.

Hii ni baada ya Bw Gachagua kuchemka na kuwazomea akiwataka waheshimiane na waheshimu umoja wa Mlima Kenya, akiongeza kwamba “hizi siasa kama za ODM hatuzitaki hapa Mlima Kenya”.

Hata hivyo, haikuwaponyoka wadadisi wa kisiasa kusoma shida kubwa katika jitihada hizo za Bw Gachagua ambapo seneta wa Kiambu Bw Karungo Thang’wa alipoapa kwamba “sisi hatutanyamazishwa na yeyote na wakati mambo yanaenda mrama tutaongea kwa uhuru wetu wa kimaamuzi”.

Katika Kaunti ya Murang’a, licha ya hali kuwa tulivu lakini ishara za kimwili zikionyesha mpasuko uliopo katika siasa za Mlima Kenya, Gachagua aliapa kuwa ataendelea kutekeleza harakati za kuwa kinara wa siasa za eneo hilo.

“Mimi nikiwa na Rais tutahakikisha kwamba siasa zetu zimelainika nyuma ya serikali yetu. Katika uchaguzi mkuu wa 2027 mimi na Rais tutakuwa pamoja na wale ambao wako na nia ya kupaa zaidi itawabidi wakuje kwanza kwetu tuwapee mawaidha na wajiepushe na siasa za migawanyiko,” akasema.

Lakini wakati Seneta wa Murang’a Joe Nyutu alipishwa kuongea, alisema kwamba “hata kichwa changu Rais, kimejaa akili”.

Hii ni baada ya kauli ya awali ya Bw Gachagua kusema kwamba “seneta Nyutu na mwenzake wa Nyeri Wahome Wamatinga wana mazoea ya kuongea matope (upuzi)”.

Bw Nyutu akishirikiana na Mbunge wa Gatanga Edward Muriu walikuwa wamemuomba Rais Ruto amtimue Bw Gachagua kutoka tiketi ya kugombea awamu ya pili ya urais na badala yake amchukue mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro kama mgombea mwenza na pia amtawaze mbunge huyo kuwa mrithi wa urais 2032.

Akiteta, Bw Wamatinga ambaye ni mwandani wa Bw Gachagua alidai kwamba Ikulu ilikuwa imehusika katika vita hivyo dhidi ya Naibu Rais na akaonya kwamba kutaandaliwa mkutano wa kutathimini upya uhusiano wa Mlima Kenya na Rais Ruto.

Mnamo Alhamisi, Bw Gachagua mbele ya kiongozi wa nchi alimzomea Bw Muriu akimtaka kwanza ajishughulishe na siasa za kuchaguliwa kwa awamu ya pili kabla ya kujiingiza kwa siasa za kitaifa.

Mmoja wa wanasiasa wanaompinga Bw Gachagua aliambia Taifa Leo kwamba ni juu ya Rais kuchagua kufuata kauli za kukandamiza watu wa Mlima kufanya maamuzi yao kwa hiari au aamue kuwapa watu nafasi wajieleze waziwazi kuhusu hisia zao kuhusu serikali yake na pia mkondo faafu zaidi wa kuelekea mbele.

“Haiwezekani kwamba mtu mmoja anasimama mbele ya mikutano na kujitawaza kama msemaji wetu pasipo kutuuliza maoni yetu na hatimaye kusema kwamba yeye ndiye atatoa ruhusa kwa wengine kupaa kisiasa,” akasema mwanasiasa huyo.

Hayo yakijiri, mrengo wa upinzani Mlima Kenya unaopata maagizo yake kutoka imani kwa Azimio la Umoja chini ya hisia za rais mstaafu Uhuru Kenyatta umezidisha juhudi zake ka kukoroga siasa za eneo hilo, Kalonzo Musyoka tayari akionekana kupiga kambi huko na aliyekuwa Gavana wa Murang’a Mwangi wa Iria akitangaza kwamba “sisi Mlima Kenya tulijikanganya kuunga mkono utawala huu wa Kenya Kwanza na 2027 tutarekebisha hali”.

Kaunti za Mlima Kenya ambazo kwa sasa ziko katika malumbano makali ya kisiasa ni Kiambu, Murang’a, Kirinyaga, Nakuru na Meru huku kukiwa na mirengo inayompinga Bw Gachagua kuwa kinara wa siasa za eneo hilo.

Murang’a ndiko ngome kuu ya uasi dhidi ya Gachagua pendekezo likiwa ni mbunge wa Kiharu, Kirinyaga tayari kukishuhudiwa shambulizi dhidi ya Mbunge mwakilishi wa Kaunti Bi Njeri Maina nayo Nakuru kukiwa na kauli za kiumng’atua gavana Susan Kihika. Katika Kaunti ya Meru vita ni dhidi ya gavana Kawira Mwangaza ambaye amejaribiwa kung’atuliwa mara mbili, akiponyoka.

Katika hali hizo zote, Bw Gachagua amekuwa akijaribu kuingilia kati lakini kukizuka minong’ono chini kwa chini kwamba hakujakuwa na uwiano wa Mlima kwamba yeye ndiye kinara wao.

[email protected]