Ruto amshambulia Kalonzo akidai si mtu mchapakazi
RAIS William Ruto Jumapili alionekana kumlenga Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka, akimrejelea kama kiongozi ambaye si mpenda maendeleo licha ya kwamba amekuwa kwa siasa kwa zaidi ya miaka 50.
Akiongea katika Kaunti ya Kiambu, Rais bila kumtaja Bw Musyoka moja kwa moja, alisema inashangaza kuwa amekuwa akipinga Hazina ya Miundomsingi ilhali barabara za kuelekea kwake ziko katika hali mbaya.
Kati ya viongozi wa upinzani, Bw Musyoka, 71 ndiye amekuwa katika siasa kwa kipindi kirefu zaidi. Pia, barabara ya kuelekea kwake Tseikuru, Kaunti ya Kitui kwa wakati mmoja iligonga vichwa vya habari kuwa hali mbaya alipotembelewa na vinara wenzake wa upinzani
Bw Musyoka alihudumu kama waziri kwenye wizara mbalimbali wakati wa utawala wa Rais Daniel Moi na pia alikuwa makamu wa rais katika utawala wa Rais Mwai Kibaki kati ya 2008-2013.
Bw Musyoka amekuwa akipinga kuanzishwa kwa Hazina ya Miundomsingi akisema kuwa inaenda kinyume cha katiba na Sheria ya Fedha za Umma.
Makamu huyo wa rais wa zamani alisema kuwa Bunge halitafuatilia na kukagua matumizi ya pesa hizo, hilo likitilia shaka uwazi katika matumizi ya pesa za umma.
Rais alishangaa ni vipi Wakenya wanamtarajia kiongozi kama huyo kumakinikia miradi ya maendeleo ilhali hawakufanya hivyo akiwa na mamlaka.
“Yeye mwenyewe, huyo mnamngojea, amekuwa kwa uongozi miaka 50. Barabara ya kwenda kwake ni ya vumbi na matope. Atatoa wapi akili, kama amekosa akili ya kupanga barabara ya kwenda kwake?” Rais Ruto akauliza.
Aliongeza kuwa kufeli kwa viongozi ndiko kumewasukuma kusema mpango huo haufanyi kazi.
“Ndio maana mnaona wanasema ati haiwezekani. Because they have never planned anything (Kwa sababu hawajawahi kupanga chochote),” akaongeza.
Rais Ruto alisema utawala wake unalenga kujenga kilomita 28,000 za barabara kufikia mnamo 2022, akiongeza barabara za kilomita 10,000 ambazo zilijengwa wakati wa utawala wa Rais Uhuru Kenyatta.
Alisisitiza kuwa mpango huo ni muhimu katika kuhakikisha Kenya inapiga hatua kiuchumi.