Siasa

Ruto atuma mawaziri ‘ground’ kumwandalia njia ya 2027

Na BENSON MATHEKA, MOSES NYAMORI December 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

MWAKA wa 2026 unaashiria kuwa wa joto kali kisiasa baada ya Rais William Ruto kuamrisha mawaziri wake kuongoza kampeni za kutetea kiti chake 2027.

Hivyo basi, Mawaziri  wamechukua usukani wa siasa katika kaunti zao, wakisukuma ajenda za serikali ya Kenya Kwanza kupitia mikakati ya kisiasa inayofichwa kama ziara za maendeleo.

“Kuanzia sasa mtatuona tukizunguka nchini zaidi kuliko awali. Ni agizo kutoka juu,” alisema waziri mmoja aliyejiuzulu ubunge mwaka jana kuingia katika Baraza la Mawaziri.

Wakijificha nyuma ya ziara za maendeleo, mawaziri wameanzisha kampeni kali za kumtetea rais huku wakizindua na kutangaza miradi ya serikali katika maeneo yao.

Baadhi ya mawaziri hawa ni wanasiasa wazoefu waliowahi kuwa wabunge au magavana kwa miaka mingi, na wanachukuliwa kuwa muhimu kwa siasa katika taifa ambalo bado linaendeshwa kwa misingi ya ukabila.

Baadhi yao walikuwa mstari wa mbele katika chaguzi ndogo za hivi majuzi ambapo serikali  jumuishi ilizoa viti vyote saba. Baada ya ushindi huo, Rais Ruto anaripotiwa kuwaagiza mawaziri wake washike usukani wa kampeni zake za 2027 katika maeneo yao.

Ngome za kisiasa za marehemu Raila Odinga, Nyanza, Pwani, Magharibi na Kisii zimo katika orodha ya maeneo yanayolengwa. Pia analenga ukanda wa Mlima Kenya, ambao ulimpa kura nyingi 2022 lakini sasa unachukuliwa kuwa umejitenga na serikali kufuatia kuondolewa kwa Rigathi Gachagua kama Naibu Rais mwaka 2024.

Katika chaguzi ndogo za Novemba 27, Naibu Rais Kithure Kindiki na Waziri wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku waliongoza kampeni za Mbeere North, huku Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi akiongoza kampeni za Malava.

Katika Ugunja, Waziri wa Kawi Opiyo Wandayi aliongoza kampeni zilizofanikisha ushindi wa upande wa serikali, na Waziri wa Madini Hassan Joho aliongoza wanasiasa wa Pwani kutwaa kiti cha Magarini.

Chaguzi hizo ndogo zilionekana kama kura ya maamuzi kuhusu utendakazi wa serikali ya Ruto, ambayo imekuwa ikipoteza uungwaji mkono tangu maandamano makubwa ya vijana nchini mnamo Juni 2024. Baada ya ghasia hizo, Rais Ruto alimgeukia Raila Odinga kumsaidia kutuliza joto la kisiasa, hatua iliyopelekea uteuzi wa mawaziri watano kutoka ODM kabla ya Odinga kufariki Oktoba.

Mikakati mipya inawaweka Prof Kindiki, Mudavadi, Wandayi, Ruku, Waziri wa Fedha John Mbadi, Waziri wa Biashara Lee Kinyanjui, na Waziri wa Ardhi Alice Wahome kama majemedari wakuu wa kampeni. Wengine ni Joho, Waziri wa Vyama vya Ushirika Wycliffe Oparanya, Waziri wa Kazi Alfred Mutua na Waziri wa Michezo Salim Mvurya.

Akiwa Siaya wikendi, Wandayi alifichua mkakati mpya akisema atasimamia kampeni za urais za Ruto katika eneo hilo. Alisema tayari amekutana na wabunge wa Siaya na wamekubaliana kumuunga mkono Ruto 2027.

“Tutachukua usukani kuongoza eneo hili kumuunga mkono Rais Ruto. Hatutaki watu wetu kupotoshwa,” alisema.

Mbunge wa Gem Elisha Odhiambo alisema Wandayi ndiye kiongozi mkuu zaidi katika Siaya na akaongeza kuwa “roho ya Raila bado inatembea hapa na tunasubiri iangukie mmoja wetu.”

Prof Kindiki naye alikutana na wabunge 60 wa Kenya Kwanza nyumbani kwake Karen kujadili namna ya kurudia ushindi wa chaguzi ndogo kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Katika kampeni za chaguzi ndogo, Prof Kindiki alijitaja kuwa msemaji mpya wa Mlima Kenya akipambana na Gachagua.

“Ni nani alimchagua kuwa msemaji wa eneo? Mimi ndiye mfalme wa mlima,” alisema.

Wakati huohuo, Mbadi ameendeleza kampeni za kushawishi jamii ya Luo kumuunga mkono Ruto, huku akifanya ziara nyingi Eldoret na katika kaunti yake ya Homa Bay.

Dkt Mutua na Joho pia wamekuwa wakizunguka Ukambani na Pwani kumpigia debe Rais Ruto.

Hata hivyo, suala la mawaziri kujihusisha na kampeni limezua mzozo katika kila uchaguzi, wapinzani wakisema ni uvunjaji wa sheria.

Seneta wa Kitui Enoch Wambua alisema hatua hiyo ni “ukiukaji wa wazi wa sheria” na akaonya kuwa kila waziri atawajibika binafsi.

Lakini Mkuu wa Huduma za Mawasiliano ya Rais, Munyori Buku, alisema mawaziri hao wanatekeleza majukumu yao ya ushirikishaji wa umma na ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo.

Katika kesi yake ya kupinga matokeo ya urais mwaka wa 2017, Raila Odinga alidai mawaziri walihusika kisiasa kinyume cha sheria, lakini Mahakama ya Juu ilitupilia mbali madai hayo, ikisema mawaziri  huteuliwa kisiasa  kutekeleza manifesto ya rais.

Mahakama ilisema ingawa Kifungu cha 23 cha Sheria ya Maadili ya Uongozi kina utata, haingekitangaza kuwa kinakiuka Katiba.