Siasa

Ruto, Gideon Moi wapigania ala za uongozi wa jamii

September 23rd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na ONYANGO K’ONYANGO

VIONGOZI wa chama cha KANU wamemshutumu Naibu Rais, William Ruto kwa kuwatumia baadhi ya wazee wa jamii ya Kalenjin kutoka kabila la Myoot kumdhalilisha Seneta wa Baringo Gideon Moi katika eneo la Bonde la Ufa.

Katibu Mkuu wa Kanu, Nick Salat aliwaongoza viongozi kukemea Dkt Ruto akirejelea tukio la hivi majuzi ambapo baadhi ya wazee wa Myoot walirejesha ala za kitamaduni za uongozi zilizokabidhiwa marehemu Rais Daniel Moi na jamii ya Nandi.

“Anatumia madai yasiyo ya kweli ya kurudisha vyombo vya uongozi. Ni familia ya Mzee Moi ambayo inaweza kurudisha vyombo hivyo lakini hakuna hafla iliyoandaliwa kwa minaajili ya sherehe hizo,” akasema Bw Salat.

“Huwezi kumsubiri Mzee Moi afariki kisha uanze kudai ulipokea vyombo vya uongozi, kutoka wapi,” akauliza.

Kauli ya Bw Salat inatokana na Baraza la Wazee wa Tugen kurejesha vyombo vya utawala Mzee Moi alikabidhiwa 1955 na wazee kutoka Nandi.

Myoot ni Muungano wa makabila yote madogo yanayojumuisha jamii ya Kalenjin. Makabila hayo ni Nandi, Kipsigis, Tugen, Marakwet, Keiyo, Pokot, Sabaot, Cherang’any, Ogiek na Terik.

Mnamo Jumapili, baadhi ya wazee, wakiongozwa na David Chepsiror walishutumu walioshiriki hafla hiyo ya kitamaduni Alhamisi iliyopita, wakisema waliohusika ni wanafiki. Wazee hao walisema haikuwa vyema kwa wenzao wa Tugen kudai walikuwa wakirejesha vyombo vya utawala vilivyokabidhiwa Mzee Moi miaka 65 iliyopita bila baraka za wazee wa Kalenjin na watoto wa Mzee Moi.

“Wazee kutoka Baringo waliosafiri hadi Sochoi, Nandi kurudisha vyombo vya utawala ambavyo Mzee Moi alipewa hawakufuata utaratibu unaohitajika. Hakuna wakati ambapo sisi kama wazee tumedai vyombo alivyokabidhiwa Mzee Moi,” akasema Mzee Chepsiror.

Ingawa hivyo, Bw Salat ambaye ni mkosoaji mkubwa wa Dkt Ruto, alisema Kanu haitajishughulisha na siasa hizo na badala yake itajikita katika kuimarisha umaarufu wake kabla ya uchaguzi wa 2022.

Mbunge huyo wa zamani wa Bomet, alisema chama hicho kitaendelea kumuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta ili atimize ajenda yake kwa Wakenya.

“Siasa zetu za kijamii au ushindani kati ya viongozi wetu, hautachangia chochote kuimarisha umaarufu wetu maeneo mengine ya nchi. Kilicho muhimu ni yale tutakayoafikia kama taifa,” akasema Bw Salat.

Kanu ilitia saini mkataba wa ushirikiano na Jubilee huku ikiwa mstari wa mbele kuunga mkono mabadiliko ya kikatiba kupitia Jopokazi la Maridhiano (BBI). Kwa upande wake, Mbunge wa Tiaty, William Kamket alifafanua kwamba, Kanu inaendeleza ushirikiano na viongozi kutoka maeneo mengine ikijipanga kwa kura za 2022.

“Si siri kwamba Kinara wetu Gideon Moi sasa analenga Urais wa nchi mnamo 2022 ndiyo maana lazima tushauriane na viongozi wengine ili kuimarisha nafasi yake ya kuingia uongozini badala ya huu ufalme wa Bonde la Ufa,” akasema Bw Kamket.

Kanu imekuwa ikiwarai viongozi waliogura kambi ya Naibu Rais, waungane nao ikilenga kuweka Bw Moi kwenye nafasi nzuri ya kuingia Ikulu 2022.

Baadhi ya wadadisi wa kisiasa wanadai Muungano wa Jubilee, Kanu na Chama Cha Mashinani kinachoongozwa na aliyekuwa Gavana wa Bomet Isaac Ruto, unaweza kuzima kabisa umaarufu wa Dkt Ruto eneo la Bonde la Ufa. Hata hivyo, wandani wa Naibu Rais wasema yeye ndiye kigogo wa siasa eneo hilo.