Sababu ya Oburu na Wandayi kutofautiana kuhusu ada za maeneo ya kupitishia nyaya za stima
PENDEKEZO la maseneta kwamba serikali za kaunti ziwe huru kukadiria viwango vya ada za maeneo ya kupitishia nyaya za stima na mawasiliano litachangia ongezeko la bei kawi hiyo na data za mawasiliano, serikali ya kitaifa imeonya.
Waziri wa Kawi Opiyo Wandayi alisema kuwa hatua hiyo itachangia kuongezeka kwa bei ya stima kutokana na ongezeko la gharama ya kuunganisha kawi hiyo.
Waziri huyo alisema serikali imekuwa ikijitahidi kupunguza bei ya stima nchini na kwamba hatua kama hiyo itahujumu juhudi hizo na hata kuchangia kuongezeka kwa viwango vya sasa vya bei ya stima.
Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Kawi ya 2025 unaodhaminiwa na Seneta wa Siaya Oburu Oginga unalenga kuzipa serikali za kaunti mamlaka ya kukadiria ada za maeneo ya kupitishia miundo msingi ya usambazaji wa stima katika maeneo yao, bila kuhitaji idhini kutoka serikali ya kitaifa.
Hii ni kupitia kufanyiwa marekebisho kwa Sehemu ya 223 ya Sheria ya Kawi ili kuondoa Serikali za Kaunti kutoka orodha ya asasi za umma zinazohitajika kupata idhini kutoka kwa Waziri wa Kawi kabla ya kutoza ada kama hizo.
Waziri Wandayi alisema athari za marekebisho hayo ya sheria zitakuwa ada zisizo sawa katika ngazi za kaunti, hali itakayochangia ongezeko la bei ya stima. Hii itahujumu mpango wa serikali wa kupunguza gharama ya kawi hii kupiga jeki ukuaji wa kiuchumi.
“Ni muhimu kuzingatia kwamba nyaya za stima hupitia kaunti tofauti zinazoongozwa tofauti na kwa kuruhusu kupitishwa kwa mswada huu serikali za kaunti zitakuwa na uhuru wa kutoza viwango vya ada zinavyotaka,” akasema Bw Bw Wandayi.
Alipofika mbele ya Kamati ya Seneti kuhusu Kawi Jumanne, Katibu wa Wizara ya Habari na Utangazaji Stephen Isaboke alisema marekebisho hayo yaliyopendekezwa yataathiri vikali sekta hiyo kwa kuchangia kuongezeka kwa gharama ya uwekaji wa nyaya za kufanikisha mawasiliano ya intaneti.
Aliiambia Kamati hiyo inayoongozwa na Dkt Oginga kwamba pendekezo hilo litachangia kuanzishwa kwa gharama mpya, hatua ambayo itachangia kuongezeka kwa gharama ya kuweka mitandao ya mawasiliano hadi katika ngazi za mashinani kote nchini.
“Hatimaye bei ya huduma za kidijitali, ada za mawasiliano, bei ya data zitaongezeka hatua ambayo itakuwa pigo kwa mpango wa serikali wa kuhakikisha kuwa maeneo yote ya nchi yanaunganishwa kwenye mitandao ya mawasiliano,” akasema Isaboke.