Siasa

Sababu za Raila kukutana na Wanjigi

January 11th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA WANDERI KAMAU

KIONGOZI wa Azimio la Umoja, Bw Raila Odinga, ameanza juhudi za kuwatafuta washirika wapya wa kisiasa, baada ya urafiki wake na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta kusawiriwa na baadhi ya wachambuzi kama ulioingia doa.

Mnamo Jumatano, duru ziliiambia Taifa Leo kuwa Bw Odinga amelazimika kuchukua hatua hiyo kutokana na mzozo unaoendelea kutokoka katika Azimio La Umoja-One Kenya, ukiwahusisha viongozi wa mrengo huo kutoka Mlima Kenya.

Hilo pia limechangiwa na ahadi ya Rais William Ruto ‘kumsaidia’ Bw Odinga kuchaguliwa kama mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AU), inayoshikiliwa kwa sasa na Mahamat Faki kutoka Chad.

Mnamo Jumanne, Bw Odinga alifanya kikao nadra na mfanyabiashara Jimi Wanjigi katika hoteli moja jijini Nairobi, hatua iliyozua maswali mengi miongoni mwa wadadisi.

Ijapokuwa ripoti kutoka mkutano huo zilieleza wawili hao walijadili kuhusu mikakati ya kuishinikiza serikali ya Kenya Kwanza kupunguza gharama ya maisha, wadadisi wanasema kuwa lengo kuu la Bw Odinga ni kutafuta washirika wapya Mlima Kenya kutokana na migawanyiko ya kisiasa inayoendelea katika Azimio la Umoja.

Kwenye migawanyiko huo, washirika wa Bw Odinga wamekosoa kubuniwa kwa vuguvugu la Kamwene, linalowashirikisha wanasiasa wa mrengo huo kutoka ukanda wa Mlima Kenya.

Kundi hilo linadaiwa kuwa na “baraka” za Bw Kenyatta, ikizingatiwa linawashirikisha washirika wake wa karibu kama kiongozi wa Narc-Kenya, Bi Martha Karua, Katibu Mkuu wa Jubilee Bw Jeremiah Kioni, aliyekuwa Waziri wa Kilimo Peter Munya kati ya wengine.

“Bila shaka, ikizingatiwa kuna mkono wa Bw Kenyatta kwenye mzozo unaoendelea katika Azimio, Bw Odinga hakuwa na uamuzi mwingine ila kumtafuta mshirika tofauti katika Mlima Kenya. Lengo kuu la uwepo wa Bw Wanjigi ni kujaza nafasi ya Bw Kenyatta,” asema Bw Martin Andati, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Bw Andati pia anataja uamuzi wa kiongozi wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka, kutangaza azma ya kuwania urais 2027 kwa tiketi ya Azimio kama sababu nyingine ya Bw Odinga kufanya kikao hicho.

Kulingana naye, Bw Wanjigi atamfaidi Bw Odinga mara mbili—kisiasa na kifedha—ikizingatiwa alijijenga kisiasa 2022, alipojaribu kuwania urais, japo akazuiwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

“Licha ya Bw Wanjigi kuzuiwa na IEBC kuwania urais 2022, ni wazi kwamba ashajijengea jina nchini. Kutokana na hilo, haitakuwa vigumu kwake kumuuza kisiasa kwa Wakenya,” asema Bw Andati.

Sababu nyingine inayotajwa kuchangia mkutano huo ni nia ya Bw Odinga kuwapatanisha Bw Wanjigi na Rais William Ruto, kwani wawili hao walikosana na kutofautiana vibaya wakati wa uchaguzi mkuu wa 2022.

“Tayari, Bw Odinga ashapatana na Rais Ruto. Bw Wanjigi ni mfanyabiashara ambaye amekuwa akipata kandarasi kutoka kwa serikali zilizopita. Hivyo, kuna uwezekano mkubwa kwamba Bw Odinga anampatanisha mfanyabiashara huyo na Rais Ruto kwa malengo ya kibiashara,” akasema mdadisi wa siasa Oscar Plato.