Sakaja adai kumshinda mwandani wa Gachagua kwa wajumbe kura za UDA Nairobi
MZOZO wa kisiasa kati ya Naibu Rais Rigathi Gachagua na Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja umeshika kasi, baada ya matokeo ya uchaguzi wa Chama cha UDA katika jiji kuu kutolewa.
Mnamo Jumamaosi, Gavana Sakaja alikutana na mrengo wake na akaupongeza baada ya uchaguzi uliokamilika katika ngazi ya wadi.
Wajumbe wengi waliochaguliwa katika nyadhifa mbalimbali waliwashinda wapinzani wao walio katika mrengo unaoungwa mkono na Bw Gachagua.
Bw Sakaja alisema wagombea wake walipata nafasi 240 kati ya 340.
“Hatutagawanywa na siasa za kikabila. Tutaungana kwa ajili ya Nairobi bora,” alisema Bw Sakaja.
Alipoendelea kusherehekea, kimya kilitawala katika kambi ya Mbunge wa Embakasi Kaskazini Bw James Gakuya, ambaye anawania uenyekiti wa UDA akiungwa mkono na Bw Gachagua.
Mwakilishi wa Wadi Nairobi Kusini Bi Waithera Chege, ambaye ni miongoni mwa maajenti wa Bw Gakuya, alishikilia kuwa mbunge huyo ndiye ataibuka mshindi katika kura ya mwisho.
“Lazima Gavana Sakaja akubali kuwa mwenyekiti wa Kaunti ya Nairobi ni Bw Gakuya, kwa sababu idadi haidanganyi.
Wanachama wa UDA, Nairobi wanasema hatoshi,” alisema Bi Chege.
Alidai kuwa baadhi ya wapiga kura waliruhusiwa kupiga kura kwa kutumia vitambulisho ambavyo ni vya watu wengine.