Seneta Murango: Siasa za Mlima Kenya zina nyota ya ‘upumbavu’
NA MWANGI MUIRURI
SENETA wa Kirinyaga Bw Kamau Murango amewasuta baadhi ya wanasiasa akidai kauli zao zinalenga kuhujumu bahati ambayo iko mikononi.
“Sisi watu wa Mlima Kenya ni watu wa ajabu. Tunavua samaki ambao tayari wako ndani ya kapu letu. Wale samaki ambao tushatoa baharini ndio tunataka kuvua wakiwa kwa kapu letu!” akashangaa.
Bw Murango alilalamika kwamba wadhifa wa Naibu Rais ni cheo cha nguvu ambacho jamii za kutoka Mlima Kenya zinafaa kujivunia.
“Tuko na mgao wa asilimia 47 ya mamlaka ya serikali ya Kenya Kwanza lakini ukisikia baadhi ya viongozi kutoka eneo hili wakilialia utatambua hatujielewi kwa kuwa tunawapiga kisiasa wale wetu walioko serikalini,” akasema Bw Murango.
Alisema kwamba hali hiyo inaangazia wenyeji wa Mlima Kenya kama walio na roho chafu ya kuhujumiana kwa msingi wa ‘wivu’.