• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:39 PM
Shinikizo zazidi Mlima Kenya kuwa na chama chake cha kisiasa

Shinikizo zazidi Mlima Kenya kuwa na chama chake cha kisiasa

NA WANDERI KAMAU

VIONGOZI zaidi wanaendelea kujitokeza kushinikiza kuwa lazima eneo la Mlima Kenya liwe na chama chake cha kisiasa ielekeapo Uchaguzi Mkuu wa 2027.

Viongozi hao wanashikilia kuwa licha ya eneo hilo kuupigia kura kwa wingi mrengo wa Kenya Kwanza, na hata kupewa nafasi nyingi za uwaziri katika serikali ya Rais William Ruto, lilifanya kosa la kutokuwa na chama chake cha kisiasa.

Kufikia sasa, baadhi ya viongozi ambao wamejitokeza kutoa kauli hiyo ni Seneta Wahome Wamatinga (Nyeri), magavana wa zamani wa Kiambu William Kabogo, Ferdinand Waititu na Dkt James Nyoro.

Mdahalo huo ulianzishwa na Bw Wamatinga, japo akakosolewa vikali na Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Mwishoni mwa Januari, Bw Wamatinga alisema kuwa moja ya sababu zilizokuwa zikichangia malumbano ya kisiasa katika ukanda huo ni ukosefu wa chama chake huru cha kisiasa.

“Tunahitaji kuwa na nyumba yetu kisiasa. Ikiwa hilo lingefanyika, sidhani tungekuwa tunashuhudia mivutano na malumbano ya kisiasa yanayoendelea kuhusu ni urithi wa uongozi wa eneo hilo. Lazima eneo hili liwe na chama kimoja kitakachowaunganisha watu wote,” akasema Bw Wamatinga.

Mnamo Jumatatu, Bw Kabogo alitoa kauli kama hiyo, akitaja hilo kuwa njia ya pekee itakayohakikisha kuwa eneo hilo limeungana kisiasa na kuimarisha usemi wake kwenye uchaguzi mkuu wa 2027.

“Ingawa eneo hili liliunga mkono Kenya Kwanza kwa asilimia 47, chama cha UDA ni kama nyumba ya wenyewe. Tunafanana na watoto wanaotafuta hifadhi katika nyumba ya jirani. Katika hali hiyo, watoto hao huwa hawana lolote, pale wanapoagizwa kutoka. Tunahitaji kuwa na chama au vyama vyetu vitakavyotuunganisha kama eneo moja,” akasema Bw Kabogo.

Kwa upande wake, Bw Waititu alishikilia kuwa moja ya malengo yake makuu ni kuhakikisha kuwa vigogo wote wa kisiasa katika eneo hilo wameungana na kubuni msimamo mmoja wa kisiasa.

“Niko kwenye juhudi za kuwaunganisha vigogo wote wa kisiasa katika eneo hili, ili kuhakikisha kuwa tuna msimamo mmoja wa kisiasa. Migawanyiko ambayo imekuwepo haitamsaidia yeyote. Kwa sasa, sote tunateseka kutokana na matatizo ambayo yamekuwepo,” akasema Bw Waititu.

Jumanne asubuhi, Bw Nyoro aliunga mkono miito hiyo, akisema kuwa changamoto za kiuchumi na kisiasa zinazolikumba eneo hilo zinatokana ukosefu wa chama kimoja cha kisiasa.

Kutokana na miito hiyo, wadadisi wa kisiasa wanasema kuwa ijapokuwa huenda hicho kikawa kibarua kigumu, kutalingana na mielekeo ambayo vigogo wa kisiasa waliopo watachukua.

“Kuna uwezekano juhudi hizo zikakumbatiwa na baadhi ya wanasiasa. Hata hivyo, yote yatalingana na ikiwa watafutilia mbali azma zao za kisiasa ili kuwaunganisha wenyeji,” asema mdadisi wa siasa Mark Bichachi.

Kulingana naye, viongozi wengi wanaotoa miito hiyo ni wanasiasa walio kwenye baridi ya kisiasa.

“Wakati wanasiasa wanapokosa kuchaguliwa, huwa wanatoa kila aina ya mashauri na mapendekezo, lakini huwa wanasahau hayo wanapochaguliwa,” akasema.

Alitaja pendekezo hilo kuwa kibarua kigumu, kwani eneo hilo halijawahi kuwa na chama chake kimoja cha kisiasa tangu kuanzishwa kwa vyama vingi vya kisiasa mnamo 1992.

“Mnamo 1992, eneo hilo lilikuwa limegawanyika baina ya wanasiasa Kenneth Matiba na Mwai Kibaki. Mnamo 2002, liligawanyika baina ya Mwai Kibaki na Uhuru Kenyatta. Ni 2013 na 2017 pekee lilipomuunga mkono kwa pamoja Uhuru. Sababu ni kuwa, Uhuru ndiye alikuwa Rais, hivyo alikuwa na uwezekano mkubwa wa kuchaguliwa. Hivyo, si rahisi kutimiza hilo,” akasema Bw Andati.

Kauli kama hiyo ilitolewa na mdadisi wa wa siasa Prof Ngugi Njoroge, aliyesema kuwa kitakuwa kibarua kigumu kwa wale wanaoshinikiza juhudi hizo.

  • Tags

You can share this post!

Watu 26 wauawa kwenye mapigano mapya Sudan Kusini

Ruto aliwahi kuniahidi kuniteua kama mgombea-mwenza 2022,...

T L