• Nairobi
  • Last Updated April 12th, 2024 4:55 PM
Sina tatizo kumuunga mkono Kalonzo kuwania urais 2027 – Raila

Sina tatizo kumuunga mkono Kalonzo kuwania urais 2027 – Raila

NA WANDERI KAMAU

KIONGOZI wa Azimio la Umoja-One Kenya Raila Odinga, amesema kuwa hana tatizo lolote kumuunga mkono kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, ikiwa atawania urais 2027.

Akihutubu Jumamosi katika Kaunti ya Kitui, Bw Odinga alisema hawezi kosa kumuunga mkono Bw Musyoka, ikizingatiwa kuwa hapo awali, kiongozi huyo amemuunga mkono mara mbili kuwania urais.

Baadhi ya washirika wa Bw Musyoka wamekuwa wakimrai Bw Odinga “kumrudishia mkono” kiongozi huyo, ikizingatiwa alimuunga mkono mnamo 2013 na 2017 kuwania urais.

Lakini Jumamosi, Bw Odinga alisema kuwa hana tatizo lolote  kuzingatia wito huo, ijapokuwa Bw Musyoka hajatangaza atawania urais.

“Kuna tatizo lolote Bw Musyoka kuwa mwaniaji urais? Sijasema hawezi kuwa mwaniaji. Ameniunga mkono, na mimi ninaweza kumuunga mkono. Bado sijastaafu kutoka ulingo wa siasa. Nikifanya hivyo nitawaambia,” akasema Bw Odinga.

Kauli ya Bw Odinga inajiri siku chache baada ya baadhi ya vigogo wa kisiasa katika mrengo wa Azimio la Umoja kutangaza azma za kuwania urais kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2027.

Tayari, Bw Musyoka ametangaza kwamba atakuwa debeni kwenye uchaguzi huo.

Kiongozi wa chama cha Democratic Action Party (DAP-Kenya) Eugene Wamalwa pia ametangaza kwamba atawania urais.

Washirika wa Bw Odinga wamekuwa wakimrai kwamba lazima awe debeni, hata ikiwa hatapata uungwaji mkono kutoka kwa vigogo wenzake wa kisiasa katika Azimio.

Juhudi za Bw Odinga kukivumisha chama chake cha ODM katika sehemu tofauti nchini pia zimeibua wasiwasi miongoni mwa washirika wake, kwamba kuna uwezekano anajitayarisha kuwania urais.

  • Tags

You can share this post!

Sitawaacha mayatima kisiasa, Gachagua asema ngomeni

Madijei wanawake wanaowatoa wanaume jasho katika kucheza...

T L