Siasa

Steve Mbogo: Serikali inamcheza Raila kuhusu uenyekiti AUC

March 16th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA WANDERI KAMAU

Mnamo Ijumaa, Bw Mbogo, aliyewania ubunge katika eneo la Starehe mnamo 2017 kwa tiketi ya ODM, alisema kuwa anaamini Bw Odinga “anachezwa na serikali ya Rais William Ruto kwamba itamfanyia kampeni kuwania nafasi hiyo”.

Kwenye mahojiano ya kipekee na Taifa Leo, Bw Mbogo alisema kwamba Bw Odinga anafaa kujihadari “ili kutopumbazwa na serikali kwa kisingizio cha kufanywa kampeni”.

“Ukweli ni kuwa, serikali inampotezea Bw Odinga muda ili asipate nafasi ya kutosha kujitayarisha kwa kinyang’anyiro cha urais 2027. Uchaguzi huo utafanyika Februari 2025, hivyo serikali itampumbaza Bw Odinga kwa karibu mwaka mmoja kwamba inamfanyia kampeni. Katika wakati huo, itakuwa imefaulu kuuvuruga na kuugawanya mrengo wa Azimio la Umoja,” akadai.

Akaongeza: “Baada ya Bw Odinga kushindwa kutwaa nafasi hiyo, serikali itatoa kila aina ya kisingizio ikionyesha jinsi ilikuwa imejitolea kumfanyia kampeni Bw Odinga. Wakati huo, itakuwa imebaki kama mwaka mmoja hivi Wakenya kushiriki kwenye uchaguzi wa 2027. Hilo linamaanisha kwamba Bw Odinga hatakuwa na muda wa kutosha kujitayarisha kufanya kampeni za kuwania urais. Atakuwa amepumbazwa kama vile alivyochezwa na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta kuwa angemsaidia kushinda urais kwenye uchaguzi wa 2022 kupitia Mpango wa Kuibadilisha Katiba (BBI).”

Hata hivyo, kauli yake imepuuziliwa mbali na baadhi ya waandani wa Bw Odinga, wanaosema kuwa kando na uungwaji mkono anaopata kutoka kwa serikali “pia anaendesha juhudi zake kujipigia debe”.

“Baba yuko mbioni pia kujifanyia kampeni. Hategemei pekee uungwaji mkono wa serikali,” akasema mbunge Junet Mohamed (Suna Mashariki), aliye pia Kiranja wa Wachache katika Bunge la Kitaifa.

Wadadisi wa siasa hata hivyo wamegawanyika kuhusu madai hayo ya Bw Mbogo.

“Muda ndiyo utakuwa mwamuzi mkuu kuhusu ikiwa ni kweli Bw Odinga anachezwa au la. Ni mapema sana kudai hivyo,” asema mdadisi wa siasa Oscar Plato.