Siasa

Tamko langu moja tu halipaswi kutumiwa na polisi kushtaki waandamanaji na ugaidi – Koome

Na CHARLES WASONGA July 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

JAJI Mkuu Martha Koome amepinga madai ya Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) kwamba matamshi yake yalichangia waandamanaji kushtakiwa kwa ugaidi.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Jumatano, Julai 23, 2025, Jaji Koome alisisitiza kuwa kauli yake kwamba waandamanaji walioketeza jengo la mahakama ya Kikuyu walitekeleza kitendo cha kigaidi, ilihusisha kisa hicho pekee wala sio maovu mengine yaliyotekelezwa na waandamanaji au wahuni kwingineko nchini.

Kwa hivyo, Jaji huyo mkuu alishikilia kuwa ODPP ni asasi huru ambayo uamuzi wake wa kuandaa mashtaka haupasi kushawishiwa na mtu yoyote.

Kulingana na Koome, ODPP haikupaswa kutaja kauli yake ilipofafanua Sheria Dhidi ya Ugaidi Jumatatu wiki hii.

“Ni muhimu kukariri kuwa Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma ni huru, inavyoelezwa katika Kipengele cha 157 (10) cha Katiba. Hii ina maana kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) hawezi kuelekezwa au kushawishiwa na mtu yeyote au mamlaka,” akaeleza Bi Koome.

“Uhuru huu pia unalindwa na miongozo ya ndani kama ile inayohusu Uamuzu wa Kushtaki,” akaongeza.

Kando na ODPP, Jaji Mkuu pia alifafanua kuwa Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) ni asasi huru katika utendakazi wake, haswa uchunguzi wa aina mbalimbali za uhalifu.

“Kwa hivyo, maamuzi yote kuhusu kuchunguza au kuwafungulia mashtaka washukiwa sharti yaongozwe na ushahidi unaoweza kuaminika na sheria husika. Maamuzi hayo hayashawishiwi na kauli au taarifa zinazotolewa hadharani na mtu yeyote, akiwemo Jaji Mkuu,” akasisiti Bi Koome.

Maelezo ya Jaji Mkuu yamejiri siku chache baada ya Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Renson Igonga kutoa maelezo kuhusu Sheria ya Kupambana na Ugaidi kufuatia ongezeko la kero kutoka kwa wananchi baada afisi hiyo kuwafungulia mashtaka ya ugaidi washukiwa wa uhalifu ulioshuhudiwa wakati wa maandamano ya Juni 25, 2025.

Afisi hiyo ilieleza kuwa vitendo vya washukiwa hao walioshtakiwa kwa ugaidi vilipangwa kwa nia ya kuzuia woga na kuhujumu shughuli za serikali, na hivyo ni ugaidi.

Aidha, Afisi ya Bw Igonga ilinukuu kauli ya Jaji Mkuu Koome alipotembelea Mahakama ya Kikuyu iliyoteketezwa wakati wa maandamano ya Juni 25, 2025.

Ni siku hiyo, Juni 26, 2025, ambapo Bi Koome alidai kuwa uharibifu uliotekezwa na wahuni katika mahakama hiyo ni makosa ya kigaidi.

Baadaye watu 37 waliokamatwa kwa tuhuma za kuteketeza jengo hilo la mahakama ya Kikuyu walishtakiwa kwa makosa ya ugaidi hali iliyotoa nafasi kwa washukiwa wengine, waliokamatwa sehemu nyingine za nchini, kushtakiwa kwa makosa hayo hayo.