'Tangatanga' Mlima Kenya wamtaka Murathe akome 'kuaibisha' Rais
Na MWANGI MUIRURI
WASHIRIKA wa Naibu Rais Dkt William Ruto eneo la Mlima Kenya, wamemtaka Naibu Mwenyekiti wa Jubilee David Murathe akome kumwangazia Rais Uhuru Kenyatta kama asiyeaminika wala kujielewa kisiasa.
Mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua, Ndindi Nyoro wa Kiharu na Alice Wahome wa Kandara walisema Jumapili kuwa Rais Kenyatta kutokana na matamshi ya mara kwa mara ya Bw Murathe, ameibuka machoni mwa umma kama asiye na msimamo wa kisiasa, asiyeaminika kuweka ahadi na ambaye ‘amechanganyikiwa’ kuhusu 2022.
Walisema kuwa Bw Murathe huenda akafikiria kuwa anamsaidia Rais kudhibiti siasa za Mlima Kenya na zile za urithi wa 2022 “lakini kwa hakika anamwaibisha Rais, anamkosesha heshima na kuzidisha kero ya wenyeji dhidi ya utawala wa Jubilee na siasa zake kuhusu uchaguzi wa 2022.”
Wakiongea katika mkahawa mmoja mjini Murang’a, watatu hao walisema kuwa Rais Kenyatta kama mtu binafsi ni “muungwana, wa kuaminika na asiyependa fitina ndogondogo.”
Rigathi alisema ameshawahi kuhudumu kama msaidizi wa Kenyatta “na ninaweza nikakuambia waziwazi bila hofu ya kujikanganya kuwa Bw Murathe hajatumwa na Rais kuyaanika ayasemayo kila mahali na kuishia kukanganya watu.”
Alisema kuwa Murathe amemewangazia Rais kama “aliyehadaa na anayeshirikisha aibu kwa Dkt Ruto kisiasa, ametangaza kuwa Rais atamuunga mkono kinara wa ANC Musalia Mudavadi, akabadilisha ngoma na kutangaza kuwa angemuunga mkono Raila Odinga kabla ya kubadili mawazo na kutangaza kuwa Rais alikuwa kwa Peter Kenneth au Waziri wa Kilimo, Peter Munya.”
Hata hivyo, Bw Murathe alipuuzilia mito hiyo akisema kuwa “mimi siko kwa Tangatanga na masuala ambayo tunapanga huko mbele kuhusu umoja na ustawi wa taifa hili hayataniwezesha kujibizana nao.”
Mbunge wa Gatanga Bw Nduati Ngugi alisema kuwa “mrengo wa Tangatanga Mlima Kenya unafaa uelewe kuwa isipokuwa ni jina la rais walitumia wakiwania vyeo vyao 2013 na 2017, hawangechaguliwa na ndio sababu wanafaa kuheshimu rais na washirika wake.”
“Ikiwa jina la Rais ndilo lilitufanya tuchaguliwe, basi linafaa kubakia la kuheshimiwa wala sio la kurejelewa kila wakati watu wanataka kutisha wengine kisiasa au kujihakikishia zawadi kutoka kwa wanasiasa wengine kwa msingi wa kuwaahidi kura za Mlima Kenya,” akasema Bw Rigathi.
Alimtaka Murathe kwanza awanie hata ikiwa ni uenyekiti wa Jubilee hata ikiwa ni katika ngazi ya wadi ndipo awe akiongea akiwa na uhalali wa kuwakilisha watu wanaojulikana.
Nyoro alisema mienendo na matamshi ya Bw Murathe, vinaashiria udalali wa hali ya juu kuhusu siasa na “amezingatia tu kulitumia jina la Rais kutafuta umaarufu eneo la Mlima Kenya.”
“Ikiwa Murathe humwakilisha Rais katika matamshi yake ya mara kwa mara, basi anafaa pia kuwa akiingia katika mitaa mbalimbali ya Mlima Kenya na katika mikutano atangaze hayo ambayo huyatangaza akiwa katika ngome za wapinzani wa siasa za eneo hili na pia katika vyombo vya habari,” akasema Nyoro.
Bi Wahome alisema ikiwa Murathe huongea kwa niaba ya Rais na anajua kuwa misimamo hiyo yake hutambulika mashinani eneo la Mlima Kenya, basi hafai kuwa na hofu ya kuandaa kikao katika uwanja wowote wa Mlima Kenya na akizingatia masharti ya Kiafya kuhusu Covid-19, aongee nao moja kwa moja, uso kwa uso.
“Mimi ni jirani wa Murathe ambaye ni mwanasiasa wa eneobunge la Gatanga na ninaweza nikakwambia waziwazi kuwa ikiwa kuna mtu ambaye hawakilishi sauti ya wenyeji kuhusu siasa, basi ni huyu Murathe,” akasema mbunge huyo wa Kandara.