• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 12:56 PM
Team Kusikiza Ground: Vuguvugu jipya la kutetea masilahi ya ‘Wanjiku’

Team Kusikiza Ground: Vuguvugu jipya la kutetea masilahi ya ‘Wanjiku’

NA CHARLES WASONGA

TAKRIBAN wabunge sita kutoka vyama vitatu wamebuni muungano mpya kuhakiki utendakazi wa serikali, wakidai upinzani rasmi umezembea.

Sita hao, wanaoongozwa na Naibu Kiranja wa Wachache Mark Mwenje, wanaoujumuisha Mbunge wa Githunguri Gathoni Wamuchomba wanasema wanalenga kuangazia masuala yanayowahusu Wakenya kama vile sakata ya uuzaji wa mbolea feki, mgomo wa madaktari, uraibu wa pombe, ushuru wa juu, na mpango tata wa kuwapeleka polisi wa Kenya nchini Haiti miongoni mwa masuala mengine.

Wanachama wa kundi hilo linalojiita ‘Team Kusikiza Ground’ au ‘Sauti ya Wanjiku’ ni Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino (ODM), Mbunge wa Sabaot Caleb Amisi (ODM), Catherine Omanyo (Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Busia, ODM), Amos Mwago (Starehe, Jubilee) na Charles Nguna (Mwingi Magharibi, Wiper).

Bi Wamuchomba aliyebuni jina ‘Team Kusikiza Ground’ alisema linajumuisha wabunge ambao wamejitolea kushinikiza serikali kushughulikia changamoto zinazowaathiri Wakenya, bila kuzingatia miegemeo yao ya kisiasa.

“Sisi ni wabunge tulioletwa pamoja sio na siasa bali madhila yanayowasibu Wakenya wakati kama huu ambapo kuna ushuru wa juu, mbolea na mbegu feki, ulevi kupindukia, mgomo wa madaktari na ule mpango wa kutuma polisi wetu nchini Haiti,” akasema Bi Wamuchomba kupitia taarifa fupi katika akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa X.

Bi Wamuchomba aliyechaguliwa kwa tiketi ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) katika uchaguzi wa 2022, ameasi baadhi ya misimamo ya chama hicho kikubwa katika muungano tawala wa Kenya Kwanza, akisema baadhi ya sera na sheria zinawaumiza raia wa kawaida.

Kwa upande wake, Bw Owino alisema yeye na wenzake wataiwekea serikali presha ishughulikie changamoto zinazowakumba Wakenya “bila kushiriki fujo kupitia maandamo”.

“Kundi hili linachukua nafasi ya kutetea masilahi ya Wakenya kwa njia mbadala bila maandamano,” akaeleza Bw Owino.

Akaongeza: “Tutaanza na kuipa presha serikali itimize matakwa ya madaktari ili waweze kurejea kazini baada ya kususia kwa siku 14. Hatutaki serikali ikae kitako kiasi kwamba madaktari watagoma kwa siku 100 ilivyofanyika mwaka 2016.”

Bw Owino alisema ni sharti serikali iwekewe shinikizo ndipo ijali masilahi ya raia kikamilifu.

  • Tags

You can share this post!

Urais Senegal: Faye amlemea mgombea wa ‘deep...

Uhaba wa maji huenda ukatumbukiza dunia kwa machafuko –...

T L