Siasa

Uganda, Tanzania zaonya Wakenya kuhusu Ziwa Victoria

September 15th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na ELIZABETH OJINA

UHUSIANO wa Kenya na majirani zake umeendelea kuharibika, baada ya Tanzania na Uganda kuungana na kuwaonya wavuvi wa Kenya waheshimu mipaka ndani ya Ziwa Victoria.

Kenya imeonekana kutii onyo hilo, ambapo Katibu wa Wizara ya Kilimo anayehusika na Uvuvi, Prof Micheni Ntiba amewataka wavuvi wa Kenya wasichokoze majirani, iwapo hawatakuwa na vibali kutoka shirika linalosimamia uvuvi nchini.

Haya yanajiri baada ya wavuvi watatu kutoweka majuma mawili yaliyopita walipokuwa wakiendesha shughuli zao kwenye Ziwa Victoria. Boti lao ilipatikana baadaye karibu na kisiwa cha Goziba na wakulima kutoka Tanzania.

Vipande vya mbao vilivyotumiwa kutengeneza boti lao tayari vimepatikana lakini wavuvi hao ambao wanaishi katika kisiwa cha Ringiti hawajapatikana. Wanaume hao wametambuliwa kama Kennedy Omondi, mwenye umri wa miaka 38, Brian Juma (22) na William Otieno (28).

“Tunapasa kuendesha shughuli zetu katika asilimia sita ya Ziwa Victoria ambayo iko ndani ya Kenya. Ni wale wenye leseni pekee ndio wataruhusiwa kuvuka hadi mataifa jirani. Msijishughulishe na uvuvi haramu,” akasema Profesa Micheni.

Alikuwa akiongea jana asubuhi alipokutana na maafisa wa idara ya uvuvi kutoka kaunti za Magharibi mwa Kenya.

Naye mwenyekiti wa Wasimamizi wa Fuo (BMU) eneo la Nyanza, Tom Guda aliwahimiza wavuvi kutoka Kenya kuwa waangalifu nyakati zote, huku akiwaonya dhidi ya kuvuka na kuingia Tanzania na Uganda.

“Tayari maafisa wa usalama wa Tanzania na Uganda wameonyesha wazi kuwa wanawachukia Wakenya. Kwa hivyo, nawahimiza wavuvi wetu kuwa waangalifu wasivuke mpaka,” Bw Guda akaeleza.