Siasa

Uhuni na ghasia zachafua kampeni za chaguzi ndogo

Na CHARLES WASONGA November 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

GHASIA ambazo zimezidi kushuhudiwa katika kampeni za chaguzi ndogo zitakazofanyika Novemba 27, 2025, zimezua hofu kwamba huenda matokeo ya kura hizo yasiakisi matakwa ya wapigakura.

Inahofiwa kwamba fujo hizo zilizogubika kampeni katika maeneobunge ya Kasipul, Malava, Mbeere Kaskazini na wadi ya Chwele/Kabuchai iliyoko Bungoma, zitachangia idadi ndogo ya wapigakura kujitokeza kuwachagua wawakilishi wao na hivyo kuhujumu demokrasia.

Kisa cha hivi punde kilitokea katika wadi ya Chwele/Kabuchai mnamo Jumamosi ambapo nusra Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya ajeruhiwe, wahuni walipovamia na kuvuruga mkutano wake wa kumpigia debe mgombeaji huru Eric Wekesa.

Bw Natembeya, aliyekuwa ameandamana na Mbunge wa eneo hilo Majimbo Kalasinga na Gavana wa zamani Wycliffe Wangamati, alilazimika kukatiza hotuba yake, polisi waliporusha vitoa machozi kuwatawanya wavamizi hao.
Magari yaliyokuwa kwenye msafara wa gavana huyo yalishambuliwa kwa mawe na vioo kuharibiwa.

Gavana huyo, ambaye ni naibu kiongozi wa chama cha DAP-K, alielekeza lawama kwa uongozi wa chama cha Ford Kenya chini ya Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula.

Chama hicho kimemdhamini Vincent Maunda kuwania kiti hicho kilichosalia wazi baada ya kifo cha diwani wa zamani James Barasa Mukhongo mnamo Agosti 4, mwaka huu.

Awali, duka moja linalomilikiwa na Bw Kalasinga mjini Chwele, lilivamiwa na mali kuporwa, tukio lililodaiwa kuchochewa kisiasa.

Mnamo Ijumaa ghasia zilishuhudiwa katika eneobunge la Malava, Kaunti ya Kakamega, kabla ya mkutano wa Muungano wa Upinzani uliopangwa kumpigia debe mgombeaji wa DAP-K Seth Panyako.

Juhudi za polisi kuzuia kufanyika kwa mkutano huo zilifeli baada ya wafuasi wa upinzani kukabiliana nao vikali. Hatimaye maafisa hao waliondoka baada ya kulemewa na mkutano huo ukaendelea katika uwanja wa Shule ya Msingi ya Malava.
“Tunajua kwamba wapinzani wetu wanapanga kuzua fujo na hivyo kuvuruga chaguzi ndogo zilizoratibiwa kufanyika Novemba 27. Wanataka kuwatumia polisi kurusha vitoa machozi ili kusababisha hofu miongoni mwa wafuasi wetu kuzuia wengi wenu kupiga kura; hasa akina mama,” akasema kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, muda mfupi baada ya mkutano huo kuanza.

Kauli yake iliungwa mkono na naibu kiongozi wa Jubilee Fred Matiang’i aliyewataka wafuasi wa upinzani ‘kulinda’ kura zao Alhamisi.

Kwa upande wake Kiongozi wa DAP-K Eugene Wamalwa alielezea imani kwamba Bw Panyako atapata ushindi mkubwa zaidi dhidi David Ndakwa wa chama cha UDA ambaye kampeni zake zinaendeshwa na msaidizi wa Rais William Ruto, Farouk Kibet, Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi na Bw Wetang’ula.

“Inasikitisha kuwa serikali sasa imeamua kutumia polisi kuvuruga mikutano yetu ilhali IEBC inanyamaza. Ninawaomba nyie watu wa Malava msimame kidete na mmpigie kura Seth Panyako awe mbunge wenu mpya,” akasema.

Katika eneobunge la Kasipul, Kaunti ya Homa Bay, watu wawili wameauawa kufikia sasa na wengine wengi kujeruhiwa kwenye makabiliano kati ya wafuasi wa mgombeaji wa ODM Boyd Were na Philip Aroko anawania kiti hicho kama mgombeaji huru.

Mnamo wiki jana, Tume ya Uchaguzi (IEBC) iliwatoza wawili hao faini ya Sh1 milioni kila mmoja na kutisha kuwazima kushiriki uchaguzi mdogo ikiwa wataendelea kuendesha kampeni za fujo.

Katika eneobunge la Mbeere Kaskazini, Kaunti ya Embu, mirengo ya upinzani na serikali imekuwa ikilaumiana, kuhusu njama ya kuzuia fujo.

Kiongozi wa chama cha Democratic Party (DP) Justin Muturi aliiandikia IEBC akilalamikia kile anachodai ni njama ya wanasiasa wa mrengo wa serikali kuwatuma wahuni kuvuruga upigaji kura katika ngome za mgombeaji wa upinzani Newton Kariuki, almaarufu, Karish.

“Tumepata habari kwamba siku ya uchaguzi wahuni wenye silaha butu watatumwa katika vituo kadhaa ambavyo ni ngome ya mgombeaji wetu kusababisha fujo ili kuwazuia wapiga kura kujitokeza,” akasema katika barua hiyo akielezea kuwa hiyo ni njama ya kuwanyima wapigakura uhuru wa kujiamulia atakayekuwa mbunge wao.

Kulingana na mchanganuzi wa masuala ya usalama Robert Musamalia idadi ndogo zaidi ya wapigakura watajitokeza katika maeneo ambako kumeshuhudiwa fujo nyakati za kampeni endapo usalama hautaimarishwa.
“Isitoshe, kulingana na visa vilivyotokea Malava wiki jana, itakuwa vigumu kwa wapiga kura wa huko kuwaamini maafisa wa polisi siku ya Alhamisi. Hii bila shaka itachangia watu wengi, hasa akina mama na wakongwe kutojitokeza kupiga kura,” anaeleza.