Uhuru, Gachagua wacheza ‘paka na panya’
WANDERI KAMAU Na JAMES MURIMI
RAIS Mstaafu Uhuru Kenyatta na Naibu Rais Rigathi Gachagua, Jumamosi, walicheza mchezo wa paka na panya, kwa kukwepa kukutana, kwenye hafla moja ya mazishi eneo la Othaya, Kaunti ya Nyeri.
Uwepo wa wawili hao katika mazishi ya aliyekuwa Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi, King’ori Mwangi, katika kijiji cha Ndugamano, Othaya, nyakati tofauti, ulizua taswira ya viongozi waliokuwa wakichezeana mchezo wa paka na panya ili kutoonana uso kwa macho.
Nyakati za asubuhi, Bw Gachagua alihudhuria hafla ya mazishi ya watu 17 waliofariki baada ya kunywa pombe ya sumu katika Kaunti ya Kirinyaga.
Mazishi hayo ya pamoja yalifanyika katika kijiji cha Kandongu, Kirinyaga, ambapo Bw Gachagua alieleza kusikitishwa kwake na maafisa wa serikali ambao wamekua wakishirikiana na watu wanaouza pombe haramu.
Kwa mara nyingine, alitoa onyo kali kwa machifu na viongozi wengine katika ngazi za mashinani, akiwalaumu kwa kulegea kazini, hali ambayo imetoa mwanya kwa uuzaji pombe haramu kuendelea katika ukanda wa Mlima Kenya.
Wakati huo (nyakati za asubuhi), Bw Kenyatta na wanasiasa kadhaa walikuwa katika hafla ya mazishi ya Bw Mwangi, ambayo yalikuwa yashaanza.
Duru zilieleza Taifa Jumapili kwamba haikujulikana kuhusu ikiwa Bw Gachagua angehudhuria mazishi ya Bw Mwangi, ikizingatiwa mnamo Ijumaa, alikuwa amezuru katika eneo hilo, akiwa pamoja na Rais William Ruto.
“Wengi hawakumtarajia Bw Gachagua kufika, kwani hafla ya Kirinyaga ilikuwa na uzito mkubwa, ikizingatiwa amekuwa akiongoza vita vya kukabiliana na pombe haramu Mlima Kenya,” akaeleza mwanasiasa mmoja.
Hata hivyo, ilipobainika kwamba Bw Gachagua alikuwa njiani kuhudhuria mazishi hayo, Bw Kenyatta na washirika wake waliondoka mara moja na kuelekea katika eneo la Kipipiri, Kaunti ya Nyandarua, kuhudhuria mazishi ya mkewe waziri wa zamani Amos Kimunya, Bi Lucy Kimunya.
Katika hafla ya mazishi ya Bw Mwangi, Bw Kenyatta hakutoa kauli yoyote ya kisiasa alipoamka kuwahutubia wenyeji.
Badala yake, alimsifia Bw Mwangi kama mtu shujaa, aliyeitolea katika kazi yake.
Alikuwa ameandamana na aliyekuwa gavana wa Nairobi, Mike Sonko, Bi Bi Anne Kananu (aliyemrithi Bw Sonko kama gavana), Waziri Msaidizi wa zamani Rachael Shebesh na aliyekuwa Naibu Gavana wa Nyeri, Dkt Caroline Karugu.
Bw Gachagua na waandani wake walifika baadaye, wakati Bw Kenyatta alikuwa ashaondoka.
Alipoamka kuwahutubia wenyeji, Bw Gachagua alisema kuwa hana tatizo lolote na Bw Kenyatta.
Akasema Bw Gachagua: “Ningependelea sana kukutana na Rais Mstaafu. Hata hivyo, nilikuwa kwenye hafla nyingine ya mazishi Kirinyaga, ijapokuwa ilichukua muda mrefu. Nimeambiwa ameondoka na kuhudhuria hafla nyingine. Nilitaka kuja kumsalimia kwani sijamwona kwa muda. Nilitaka kumwambia kwamba hali ni shwari na hakuna tatizo lolote lililopo. Ni mtoto na ndugu yetu.”
“Tulikuwa na tofauti ndogo, lakini hayo yameisha. Uchaguzi ulipita na tuna serikali mpya. Yeye ni kiongozi wetu. Nilitaka kumwambia tunampenda na tunamwombea,” akaongeza.
Wawili hao walitofautiana vibaya kwenye Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, 2022.
Hapo awali, duru ziliiambia Taifa Jumapili kwamba juhudi kadhaa za kuwapatanisha viongozi hao zimekuwa zikigonga mwamba.