Siasa

Vigogo wa siasa Mlimani waendeleza kimya ‘wakipima hewa’ kuhusu 2027

Na COLLINS OMULO January 15th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

HUKU wakikabiliwa na wakati mgumu, vigogo kadhaa wa siasa kutoka eneo la Mlima Kenya wanaendelea kunyamaza na ‘kupima hewa’ kuelekea uchaguzi wa 2027.

Viongozi hao, wengi wao wakiwa magavana wa muhula wa kwanza, wamechukua msimamo wa tahadhari wakikabiliwa na uamuzi mgumu wa kisiasa kati ya kumuunga Rais William Ruto au aliyekuwa rafiki yake aliyegeuka mpinzani mkuu, Rigathi Gachagua.

Wakitambua athari za maamuzi yao hasa ikizingatiwa hatima ya kuchaguliwa tena, viongozi hao wanaendelea kusubiri huku wakitafakari hatua ijayo kisiasa.

Baadhi yao ni pamoja na Gavana wa Murang’a Irungu Kang’ata, mwenzake wa Kiambu Kimani Wamatangi, Gavana wa Nyandarua Kiarie Badilisha na Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro.

Wote walichaguliwa kwa tiketi ya chama cha UDA cha Rais Ruto katika uchaguzi wa 2022 lakini sasa wamejipata kwenye mtego wa kisiasa kuhusu mwelekeo wao ujao.

Mgogoro kati ya Gachagua na mkubwa wake wa zamani unaonekana kuchafua siasa za eneo hilo lenye kura nyingi, huku wanasiasa wakiamua kuzingatia tahadhari ili kuepuka kuweka hatarini nafasi zao za kuchaguliwa tena mwaka wa 2027.

Ingawa viongozi kadhaa tayari wamechukua misimamo, magavana wa muhula wa kwanza na wabunge kadhaa wanaendelea kuchelewesha uamuzi wao.

Kati ya kaunti 10 za Mlima Kenya —Laikipia, Tharaka-Nithi, Murang’a, Kiambu, Nyeri, Kirinyaga, Nyandarua, Embu, Meru na Nakuru — kuna magavana sita wa muhula wa kwanza, ambapo ni wawili pekee kutoka Nakuru na Embu ambao wamejitokeza wazi kumuunga mkono Rais Ruto.

Akizungumza hivi majuzi wakati wa mazishi ya mamake Mbunge wa Embakasi North James Gakuya eneo la Murang’a, Gavana Kang’ata aliwaacha wengi wakijiuliza anamuunga nani, akisema ni wananchi watakaomwelekeza.

“Watu wanauliza niko upande gani wa kisiasa. Mimi ni mtumishi wenu na ni ninyi mtakaonipa mwelekeo. Nina kura moja tu na mnafahamu kuwa chaguo la wananchi ni chaguo la Mungu,” alisema gavana huyo wa muhula wa kwanza.

Hali kama hiyo ilijitokeza pia kwa mwenzake wa Nyandarua wakati wa mazishi ya babake Mbunge wa Kipipiri Wanjiku Muhia, alipoongea kwa lugha ya mafumbo.

“Nilitia saini mkataba na watu wa Nyandarua mwaka wa 2022 na wanajua waliniambia nini. Watakachoniambia kufanya siku zijazo ndicho nitafuata kwa sababu sisi ni watu tunaoheshimu mikataba,” alisema Gavana Badilisha.

Bw Nyoro ametajwa kama “mpweke kisiasa” ambaye amekuwa akikosoa serikali ya sasa baada ya kutofautiana kwake na Rais Ruto.

Hata hivyo, mbunge huyo wa muhula wa pili amekuwa akiepuka siasa za upande mmoja, akilenga zaidi masuala ya utawala nchini.

Mkakati huo ulimlazimu Bw Gachagua kumsuta hadharani, akimtaka atangaze msimamo wake wa kisiasa.

Bw Gachagua amekuwa akionya viongozi wa Mlima Kenya kuamua mustakabali wao wa kisiasa, wakati mmoja akiwapa hadi Februari 2025 wajitokeze hadharani au wakabiliwe na athari za uvuguvugu wa kisiasa.