Viongozi wa Agikuyu Rift Valley wamtaka Ndindi Nyoro kuwa na subira
NA EVANS JAOLA
JAMII ya Agikuyu katika eneo la Bonde la Ufa inayoegemea upande wa Naibu Rais Rigathi Gachagua, imemtaka Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro awe na subira badala ya kufyatuka mapema na kumezea mate nafasi ya kuwa mgombea mwenza wa Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu wa 2027.
“Tunamshauri Bw Nyoro kuweka zingatio kwa kazi yake ya ubunge badala ya kutaka kutimka mbio asizoziweza. Yeye angali kinda kisiasa hivyo afahamu mazuri yanamsubiri,” akasema Katibu wa Jamii ya Agikuyu eneo la Bonde la Ufa John Njuguna.
Bw Njuguna akihutubu mjini Kitale akiwa na wanajamii wengine, alisema ni makosa makubwa kwa viongozi wa jamii hiyo ya Agikuyu kumdunisha Naibu Rais.
Kauli ya wanajamii hao inajiri baada ya Seneta wa Murang’a Joe Nyutu kudai kwamba Bw Gachagua amegeuka kuwa tishio kwa viongozi wengi Mlima Kenya kupitia “kuwadunisha, kuwakanyagia, kuwaaibisha mbele ya Rais na wafuasi wao na pia kuwasemasema vibaya katika mikutano yake ya siri”.
Katika msingi huo, Bw Nyutu anasema kwamba ana ufuasi mkuu wa wapigakura nyuma yake na maafikiano kati ya wanasiasa wengi Mlima Kenya ni kumtaka Rais Ruto akiwania awamu ya pili mwaka 2027, amteme Bw Gachagua kama mgombea mwenza wake na badala yake amteue mwanasiasa mwingine, kwa sasa akimpendekeza Bw Nyoro.
Walimkemea Bw Nyutu na viongozi wengine wanaompinga Bw Gachagua kwa kuleta mchecheto wa kisiasa usiofaa.
“Hao wanaomdunisha Bw Gachagua wameonyesha madharau kwa ofisi ya Naibu Rais na tuko hapa kuwakemea,” akasema Bw Njuguna, ambaye aliwania kiti cha ubunge Cherangany kwa tiketi ya kujitegemea bila mafanikio.
Naye Stephen Githinji kutoka Kaunti ya West Pokot alisema hofu yake ni kwamba malumbano hayo yataua umoja wa kijamii na hata kuing’oa kutoka kwa mbio za urais.
“Bw Gachagua ni kiongozi wa kitaifa anayefaa kuheshimiwa. Tunamuunga mkono huku tukiwataka wasiompenda waache kuiweka jamii hatarini kwa kumpiga vita,” akasema Bw Githinji.
Mwingine aliyekosoa Bw Nyutu na mrengo wake ni Bi Margaret Wahito.
“Wanasiasa wanaompinga Naibu Rais wanafaa kufahamu kwamba kwa kufanya hivyo hakuna hadhi wanayopanda. Wanafaa kumpa sapoti Bw Gachagua jamii nzima ifaulu,” akasema Bi Wahito.