• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 1:08 PM
‘VIONGOZI WA KESHO’: Kaulimbiu ya UhuRuto ya kuwapa vijana kazi ilivyofeli

‘VIONGOZI WA KESHO’: Kaulimbiu ya UhuRuto ya kuwapa vijana kazi ilivyofeli

Na CHARLES WASONGA

TANGU taifa hili lipate uhuru vijana wamekuwa wakitajwa kama, “viongozi wa kesho”, lakini ‘kesho’ hiyo haifiki kwa maelfu ya vijana walioelimika na wenye uwezo wa kutwaa nafasi za uongozi serikalini. 

Wimbo ulikuwa huo huo wakati wa utawala wa Rais wa kwanza Hayati Mzee Jomo Kenyatta, na enzi za uongozi wa marais wastaafu Daniel Moi na Mwai Kibaki na sasa Rais Uhuru Kenyatta na serikali yake ya Jubilee.

Lakini wakati wa kampeni kuelekea chaguzi za miaka ya 2013 na 2017, Rais Kenyatta na Naibu wake William Ruto waliahidi kuwa serikali yao ingewapa vijana nafasi katika asasi kuu.

“Kwa sababu sisi ni viongozi vijana, tutawateua vijana katika serikali yetu kwani wao ndio wengi. Tofauti na mtizamo wa hapo zamani uliowachukulia vijana kuwa viongozi wa kesho, chini ya serikali ya Jubilee vijana watakuwa viongozi wa sasa,” Rais Kenyatta akakariri katika moja mikutano yake ya kampeni kuelekea uchaguzi mkuu 2017.

Lakini kinaya ni kwamba Rais na Naibu wake wamekuwa wakiwateua wanasiasa wazee kushikilia nyadhifa katika serikali yao tangu walipoingia mamlakani 2013. Hali hii imeshuhudiwa zaidi, hasusan, katika Bodi za Mashirika ya Serikali.

 

Muthaura (71)

Na hivi majuzi, Rais Kenyatta alimteua aliyekuwa Mkuu wa Utumishi wa Umma Balozi Francis Muthaura kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Halmashauri ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA), kuashiria kuwa serikali yake bado haijajitolea kuwapa vijana nafasi ya kuhudumu katika nyadhifa za juu.

“Ni aibu kwamba japo kuna Wakenya wengi wenye umri wa chini ambao wamehitimu kushikilia nyadhifa kama hizi, Rais Uhuru bado anaendelea mtindo huu wa kuwateua wazee na wandani wake wa kisiasa. Wengine wao wamehudumu katika utumishi wa umma kwa miongo mingi,” akasema mchanganuzi James Mwamu.

“Inaonekana kuwa wakongwe ndio wanapendelewa zaidi katika serikali hii,” akasema Mwamu ambaye ni wakili.

Muthaura, 71, ambaye atahudumu kwa muda wa mwaka mmoja hadi Oktoba 20 mwaka 2019, atafanyakazi na wanachama wengine wapya wa bodi hiyo kama vile Charles Makori Omanga, Mukesh Shah, Leonard Ithau na Dkt Susan Mudhune.

Uteuzi wa Muthaura ulikuwa umekabiliwa na changamoto kwa muda mfupi pale Mahakama ya Uajiri na Leba ilipousimamisha kwa muda. Hata hivyo, agizo hilo liliondolewa na sasa Bw Muthaura na wenzake wanne wanaweza kuchukua nyadhifa zao katika Bodi ya KRA.

Uteuzi wa Muthaura pia umepinga na viongozi wa mashirika ya umma wakisema wale watu ambao wamefikisha umri wa kustaafu wanapaswa kukataa teuzi hizo.

“Watu humu nchini wanafaa kuendeleza utamaduni, ulioko katika mataifa ya nje, ya kukataa vyeo vya umma ili kutoa nafasi kwa watu wengine.

Ikiwa umehudumu katika cheo fulani kwa miaka mingi, walivyofanya wazee hawa wa rika la Muthaura, ni bora kustaafu kwa heshima. Mbona watu huhisi kutokuwa salama kiasi kwamba hata baada ya kustaafu wao hutaka kuendelea kushikilia nyadhifa za umma?” akauliza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Sera na Utatuzi wa Mizozo (ICPC), akasema.

 

Njiraini (60)

Ajabu ni kwamba Bw Muthaura atakuwa akifanya kazi na Kamishna Mkuu John Njiraini ambaye pia ametimu umri wa kustaafu.

Mwanaharaka Okiya Okoiti Omtatah aliwasilisha kesi mahakama akidai kuwa Bw Njiraini alipaswa kuondoka afisini mnamo Machi 4, 2017 kwani angetimu umri wa miaka 60 Desemba, 2017.

Bw Njiraini alitimu umri wa kustaafu, wa miaka 60, mnamo Desemba 2017, ingawa kandarasi yake ilifaa kukamilika Machi mwaka huu. Anasalia afisini kama Kamishna Mkuu wa KRA hadi mahakama itakapotoa uamuzi kuhusu kesi ya Bw Omtata mnamo Juni 22 mwaka huu.

Na mnamo Machi mwaka huu, Bw Omtata alipata agizo la mahakama iliyosimamisha amri ya Mkuu wa Utumishi wa Umma Joseph Kinyua ulisema kuwa Maafisa Wakuu wa Mashirika ya Serikali hawapasi kustaafu wakitimu miaka 60, sawa na watumishi wengine wa umma.

Hii ilimaanisha kuwa Bw Njiraini angeweza kuteuliwa kwa muhula mwingine licha ya kutimu umri wa miaka 60 na tayari amehudumu kwa mihula miwili.

Bw Kinyua mwenyewe bado yuko afisini licha ya kutimu umri wa miaka 66.

Naye aliyekuwa Katibu wa Wizara ya Elimu Profesa Karega Mutahi ana umri wa zaidi ya miaka 70 lakini bado yuko katika utumishi wa umma.

Ndiye mwenyekiti wa Kamati ya Kiufundi ya Kushirikisha Mahusiano kati ya Serikali Kuu na zile za Kaunti (Intergovernmental Relations Technical Committee-IGTRC). Asasi hiyo ndio ilichukua nafasi ya Halmashauri ya Mpito (TA) na huongoza mchakato wa ushirikiana na mashauriano kati ya ngazi hizi mbili za serikali.

 

Obure (74), Madoka (75)

Isitoshe, katika mageuzi katika baraza la mawaziri ambayo Rais Kenyatta alifanya majuzi, kwa kubuni nyadhifa za waziri msadizi, alimteua aliyekuwa Seneta wa Kisii Chris Obure, 74, kuwa Waziri Msaidizi wa Wizara ya Uchukuzi, Miundo Mbinu, Nyumba na Ustawi wa Miji.

Katika Halmashauri ya Bandari Nchini (KPA), Rais alimteua Meja mstaafu Marsden Madoka, 75, kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya halmashauri hiyo.

Kulingana na Bw Wainaina, huu mtindo wa kurejesha wazee katika utumishi wa umma unaashiria kuwa hizi ahadi za kuwapa vijana nafasi serikalini ni siasa tupu.

“Ni jinsi gani taifa hili litaweza kukabiliana na tatizo za ukosefu wa usawa wa kiumri katika teuzi za serikali ambapo idadi kubwa ya vijana walioelimika na kuhitimu vizuri hawapewi nafasi ya kutumikia nchi yao?”, akauliza Bw Wainaina.

Kwa bahati mbaya, anaongeza Bw Wainaina, mapendeleo kwa misingi ya kisiaasa (patronage) na haja ya kuwatunuku marafiki na wafuasi ndizo vigezo ambazo huzingatiwa kabla ya teuzi hizo kufanywa.

You can share this post!

Mhubiri ajitetea kuwataka waumini wamnunulie ndege ya Sh5.4...

KIMYA CHA ‘BABA’: Raila aeleza sababu ya...

adminleo