Vyama vya Ruto na Uhuru kukabana uchaguzini baada ya kuidhinisha ndugu wa familia moja
MAPAMBANO mapya ya kisiasa yanatarajiwa kati ya vyama vya Rais William Ruto na mtangulizi wake Uhuru Kenyatta kwenye uchaguzi mdogo wa eneobunge la Isiolo Kusini, baada ya vyama hivyo kuidhinisha ndugu wa familia moja kuwania.
Watoto wawili wa marehemu Mbunge Mohamed Tubi Bidu watamenyana katika kinyang’anyiro kitakachosheheni masuala ya urithi wa kisiasa wa kifamilia, mabadiliko ya miungano ya vyama na ushawishi mkubwa wa siasa za koo katika eneo hilo.
Uchaguzi huo mdogo utafanyika Februari 26.
Mgombeaji wa United Democratic Alliance (UDA) Tubi Mohamed Tubi, atachuana na mgombea wa Chama cha Jubilee Mohamed Bina Tubi.
Wawili hao ni wana wa marehemu Bidu aliyechaguliwa kwa tiketi ya Jubilee mwaka 2022.
Bidu alifariki Novemba iliyopita akipokea matibabu katika hospitali ya Nairobi Hospital.
Katibu Mkuu wa Jubilee, Jeremiah Kioni, alipomkabidhi Bi Bina tiketi ya chama hicho ambacho kinara wake ni Bw Kenyatta, alisema Jubilee inalenga kurejesha kiti ambacho inakichukulia kuwa sehemu ya urithi wake wa kisiasa.
“Kiti hiki kilikuwa cha mbunge wa Jubilee na alikuwa mwaminifu kwa chama. Tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha tunashinda,” alisema Bw Kioni na kutaja kura hiyo kama heshima kwa uaminifu wa marehemu, na pia mtihani wa uthabiti wa chama cha Jubilee.
Kwa kinara Uhuru Kenyatta ushindi utatoa ishara ya kufufuka kwa chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027, na kuonyesha kuwa bado kinaweza kutetea ngome zake za jadi licha ya wanachama kuhama na migawanyiko ya ndani kwa ndani.
Kwa upande mwingine UDA itategemea ushawishi wa Rais Ruto.
Bw Tubi alipokea cheti chake cha uwaniaji kupitia UDA mwezi jana baada ya viongozi wa chama kueleza kuwa uteuzi huo wa moja kwa moja uliafikiwa kwa makubaliano.
“Kiongozi wa chama anashukuru viongozi na wakazi wa Isiolo kwa makubaliano ya kuunga mkono mgombeaji mmoja Tubi Mohamed Tubi na kuonyesha imani yao katika UDA,” alieleza Katibu Mkuu wa UDA, Hassan Omar, wakati wa hafla hiyo.
Mbali ushindani wa vyama siasa za koo pia zitakuwa na mchango mkubwa katika kuamua mshindi.
Kaunti ya Isiolo ina wakazi wengi wa jamii ya Borana, huku Wasomali wakiwa wachache.
Bi Bina amejaribu kujitofautisha na kaka yake, akitilia shaka mizizi ya Bw Tubi katika eneo la Isiolo Kusini.
Aliongeza kuwa Rais anajitolea kuboresha maisha ya wananchi kupitia miradi maalum ya maendeleo, akisema kuwa maeneo ya Kaskazini mwa Kenya yako katika ajenda kuu ya serikali.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na Seneta wa Isiolo Fatuma Dullo na aliyekuwa Mbunge wa Isiolo Kaskazini Charfano Mokku, jambo lililoashiria umuhimu wa kisiasa wa uchaguzi huo kwa UDA.
Mbali ushindani wa vyama, siasa za koo zinatarajiwa kuwa na uzito mkubwa katika kuamua mshindi. Kaunti ya Isiolo inaongozwa na jamii ya Borana, huku Wasomali wakiwa wachache.
Bi Bina amejaribu kujitofautisha na kaka yake, akitilia shaka mizizi yake katika eneo la Isiolo Kusini.
“Yeye anatoka Isiolo ya Kati na hakuzaliwa katika eneo hili. Hata lugha ya wenyeji haizungumzi,” alisema.
Akijitambulisha kama mrithi wa kisiasa wa baba yake, aliongeza: “Kama binti mkubwa wa marehemu, nitafanya kila niwezalo kuhakikisha ninalinda urithi wa baba yangu na kuwatumikia wakazi wa Isiolo Kusini.”
Kwa kiongozi wa Jubilee Uhuru Kenyatta, ushindi katika uchaguzi huu mdogo utakuwa ishara muhimu ya kufufua hadhi ya chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027, na kuonyesha kuwa bado kinaweza kutetea ngome zake za jadi licha ya changamoto za wanachama kuhama na migawanyiko ya ndani.