Vyama vya UDA na ODM vyang’ang’ania wanachama
NA LUCY MKANYIKA
JOTO la kisiasa katika Kaunti ya Taita Taveta linazidi kuchemka, huku vyama vya UDA na ODM vikizidi kuvutia wanachama wapya kujiandaa kwa uchaguzi wa 2027.
Licha ya kuwa uchaguzi mkuu ujao upo mbali, vyama hivyo vinaendelea kujipanga vikizingatia umuhimu wa kuwa na idadi kubwa ya wanachama upande wao ili kupata wawakilishi katika viti mbalimbali vya uongozi.
Kihistoria, kaunti hiyo imekuwa ngome ya ODM.
Hata hivyo, chama hicho kinachoongozwa na kinara wa upinzani Raila Odinga, kilipoteza nyadhifa nyingi za viti katika uchaguzi uliopita na kujizolea wawakilishi watano pekee kati ya viti 20 vya wadi na seneta Jones Mwaruma aliyechaguliwa chini ya chama hicho.
Kurejesha hadhi yake, mwezi uliopita, Bw Odinga alizuru kaunti hiyo na kuzindua zoezi la usajili wa wanachama wa ODM, akiwataka wakazi kujiunga na chama chake na kuunga mkono ajenda yake ya kuleta mabadiliko nchini.
Ikiwa na wanachama 39,400 katika kaunti hiyo, ODM inakabiliwa na ushindani mkubwa kubwa kutoka kwa chama cha UDA, ambacho sasa kinadai kusajili zaidi ya wanachama 60,000.
Ili kukabiliana na zoezi la usajili la ODM, wiki jana viongozi wa UDA katika kaunti hiyo walikutana mjini Voi ili kupanga mikakati ya usajili wa wanachama na kuendeleza umaarufu wa chama hicho katika kaunti hiyo kwa nia ya kuwavutia wakazi zaidi.
Chama cha UDA kina mwakilishi mmoja wa bunge la kaunti aliyechaguliwa na mwingine mmoja aliyeteuliwa na chama.
Bi Lydia Haika, mwakilishi wa wanawake pia alichaguliwa kupitia tiketi ya chama hicho.
Mratibu wa UDA Taita Taveta, Milton Masale alisema kuwa chama hicho kinaendelea kupata umaarufu katika ukanda wa pwani na kutakuwa chama bora kwa watu wa eneo hilo.
Bw Masale pia alisema utawala wa Kenya Kwanza unaoongozwa na Rais William Ruto umetetea ya wananchi wa chini na vilevile swala la kiuchumi.
Aliwataka wenyeji kuunga mkono serikali inapoendelea kuboresha maisha ya wakaazi.
“Gharama ya maisha inashuka na hiyo ni pongezi kwa Rais wetu. Kwa hiyo imekuwa rahisi kwetu kuwashawishi watu kujiunga na chama. Uandikishaji wa wanachama haujaanza leo, ni zoezi tunaloendelea nalo,” alisema.
Alisema viongozi wa UDA pia watashirikiana kujenga chama hicho.
“Tumeweka kando tofauti zetu na tumekubali kufanya kazi kwa pamoja chini ya mwakilishi wetu Bi Haika,” alisema.
Mwenyekiti wa kaunti wa chama cha ODM, Bw Ginton Mwachofi alisema usajili huo unafanywa katika ngazi ya wadi.
Bw Mwachofi alisema kuwa wakazi wamepoteza imani na utawala wa sasa kutokana na gharama ya juu ya maisha na kutotekelezwa kwa ahadi walizopewa wakati wa kampeni.
“Kuna wanachama wa Kenya Kwanza wanaohamia ODM. Wanahama kwa sababu Kenya Kwanza imewakatisha tamaa ya kutekeleza waliyoahidi,” alisema.
Alisema wale waliokuwa wametoka ODM wakati wa uchaguzi mkuu wa 2022 wameanza kuonyesha nia ya kurejea.
“Wengine walikuwa wamejitoa kwa sababu ya mchanganyiko wa uteuzi wa wagombea katika muungano wa Azimio. Tunalenga watu wengi iwezekanavyo haswa vijana kwa sababu baadhi yao si wanachama wa chama chochote cha siasa,” alisema Bw Mwachofi.