Siasa

Wadau wapinga baadhi ya mapendekezo kwenye mswada wa marekebisho ya sheria ya IEBC ya 2024

April 21st, 2024 Kusoma ni dakika: 3

SAMWEL OWINO Na CHARLES WASONGA

WADAU kadha wamepinga baadhi ya mapendekezo yaliyomo katika mswada unaolenga kuleta mabadiiliko katika jinsi Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inavyoendesha chaguzi kuu nchini.

Mswada huo wa Marekebisho ya Sheria ya IEBC ya 2024 unadhaminiwa na kiongozi wa wengi katika Bunge la kitaifa Kimani Ichung’wah na kiongozi wa wachache Opiyo Wandayi.

Ni mmojawapo wa fii  miswada tisa inayolenga kutekeleza mapendekezo yaliyoko kwenye ripoti ya Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo (Nadco).

Miongoni mwa wadau waliofika mbele ya Kamati ya Pamoja ya Bunge la Kitaifa na Seneti kuhusu Haki na Masuala ya Kikatiba ni wawakilishi kutoka IEBC, Idara ya Mahakama, Afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa na Tume ya Mageuzi ya Sheria  Nchini (KLRC).

Wengine walikuwa wawakilishi wa Baraza la Makanisa Nchini (IRCK), Kamati Shirikishi kuhusu Vyama vya Kisiasa (PPLC) huku jopo la uteuzi wa makamishna wa IEBC likituma memoranda.

Akiwasilisha mapendekezo yake mbele ya kamati hiyo ya pamoja, Afisa Mkuu Mtendaji wa IEBC Marjan Hussein Marjan alipinga sehemu ya mswada huo unasema kuwa Naibu Mwenyekiti wa IEBC au mwanachama yeyote anaweza kutekeleza majukumu ya mwenyekiti endapo kiti hicho kutasalia wazi.

Bw Marjan alisema uteuzi wa mwenyekiti uendeshwa na kuchapishwa tofauti na hivyo naibu mwenyekiti au kamishna yeyote hawezi kutekeleza majukumu ya mwenyekiti endapo kiti hicho kitasalia wazi.

Aidha, afisa huyu mkuu mtendaji alisema muda wa kuhudumu wa sasa wa miaka mitano kwa mshikilizi wa afisi hiyo unapasa kudumishwa au ugeuzwe kuwa muhula mmoja wa miaka sita.

Bw Marjan alipendekeza hivyo, kujibu pendekezo kwenye mswada huo kwamba muda wa kuhudumu wa afisa mkuu mtendaji wa IEBC upunguzwe hadi miaka mitatu.

“Masuala ya uchaguzi ni magumu na changamano na humchukua mtu hadi miaka miwili kuyaelewa kikamilifu. Hii ndio maana napendekeza kuwa kipindi cha kuhudumu cha miaka mitano kidumishwe au kiwekwe kuwa kipindi kimoja cha miaka sita. Miaka mitatu inayopendekezwa kwenye mswada huu ni mfupi zaidi,” akaeleza.

Msajili wa Vyama vya Kisiasa Anne Nderitu pia aliunga mkono kauli ya Bw Marjan akisema kuwa muhula wa kuhudumu kwa Afisa Mkuu Mtendaji wa IEBC unapasa kusalia kuwa miaka mitano “ili kuimarisha usalama wa kikazi na uhuru wa afisi hii.”

“Humchukua mtu angalau miaka miwili kuelewa masuala ya uchaguzi na hivyo mkiweka kipindi cha kuhudumu cha afisa mkuu kuwa miaka mitatu inamaana muda mfupi baada yake kujizoesha na kazi anakuwa akijipanda kuondoka,” akaeleza.

“Aidha, ikizingatiwa kuwa kazi ya IEBC ni kuendesha uchaguzi, kuanisha mipaka na kuendesha kura za maamuzi, afisa mkuu anafaa kutekeleza kazi nyingi za maandalizi ya shughuli hizi.” akaongeza.

Kuhusu pendekeza la kuongezwa kwa wanachama wa jopo la kuteua makamishna wa IEBC kutoka saba hadi tisa Bw Marjan alisema hatua hiyo bado haitahakikisha wadau wote wanajumuishwa, ilivyotarajiwa.

“Kuna uwezekano mkubwa kwamba nafasi nyingi bado zitaendea tabaka la wanasiasa kupitia vyama vya kisiasa,” Bw Marjan akaeleza.

“Kwa mfano mswada huo ukipitishwa idadi ya wawakilisha wa PPLC itapanda kutoka mmoja ilivyo sasa hadi watatu. Na ukiongezea wawilishi wawili wa Tume ya Huduma za Bunge (PSC) ambao bado wanatoka vyama vya kisiasa, pendekezo hilo haliafiki lengo lake la kuhakikisha wadau wote wanawakilishwa kwa usawa,” akaongeza.

Bw Marjan alipendekeza kuwa jopo la kuteua mwenyekiti na makamishna wa IEBC linapasa kujumuisha wadau wote watakaoongeza thamani kwa mchakato huo.

Afisa huyo pia alipinga pendekezo kwamba idadi ya chini kabisa ya makamishna wanaohitajika kufanya maamuzi makuu iliwa tano.

Idara ya Mahakama pia ilisema mswada huo haujashughulikia masuala yaliyoibuliwa na Mahakama ya Juu wakati wa uamuzi wake wa kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi.

“Mswada huu haujaelezea waziwazi kuhusu majukumu ya mwenyekiti wa uchaguzi, makamishna, afisa mkuu na wafanyakazi wa tume kuhusiana na shughuli nzima ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi,” akasema Msajili Mkuu wa Idara ya Mahakama Winfridah Mokaya.

Bi Mokaya aliwaambia wabunge kuandaa mageuzi ya sheria yanayooana na mapendekezo ya Mahakama ya Juu iligundua dosari kuu katika usimamizi wa IEBC.

Tume ya Mageuzi ya Sheria Nchini ilionya dhidi ya kuwekwa kwa idadi ya makamishna hitajika kuendesha shughuli kihalali kuwa watano, ikisema hali hiyo itakwamisha shughuli endapo idadi ya makamisha itapungua hadi chini ya tano.

Hata hivyo, Afisi ya Mwanasheria Mkuu iliunga mkono mswada huo ikisema haijakiuka Katiba kwa njia ya yoyote.

Naye mwenyekiti wa Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Haki na Masuala ya Kikatiba (JLAC) George Murugara alisema hakuna sheria inayosema kuwa lazima wazingatie pingamizi au mapendekezo yote kutoka kwa wadau wakati wa kuandaa nakala ya mwisho ya mswada huo wa marekebisho ya sheria ya IEBC.