Wamuchomba adai Mlima Kenya hawajaonja matunda ya KKA
NA WANDERI KAMAU
MBUNGE wa Githunguri Gathoni Wamuchomba, ameikosoa vikali serikali ya Kenya Kwanza inayoongozwa na Rais William Ruto, akisema kuwa imewahadaa wenyeji wa Mlima Kenya kuhusu ahadi ambazo ingewatimizia.
Akihutubu Jumatano katika eneobunge lake kwenye hafla moja ya mazishi, Bi Wamucomba alisema ahadi nyingi ambazo serikali ya Kenya Kwanza ilitoa, hasa uboreshaji wa sekta ya kilimo, hazijatimizwa hata kidogo tangu ilipochukua uongozi mnamo Septemba 13, 2022.
Mbunge huyo alirejelea malipo kwa wakulima wa kahawa, akisema kuwa licha ya kuahidiwa na serikali kwamba yangeboreshwa, hawajalipwa hadi sasa.
Bi Wamuchomba pia alikosoa sera ya ujenzi wa nyumba za bei nafuu inayoendeshwa na serikali, akisema inatekelezwa kimabavu, kwani nyumba hizo zinajengwa kwenye “ardhi zilizochukuliwa kwa nguvu kutoka kwa raia”.
“Serikali hii imejaa uwongo. Iliwahadaa watu wetu kwamba ingeboresha maisha yao, lakini haijafanya hivyo hata kidogo. Iliwahadaa wakulima wa kahawa kuwa ingeboresha bei za zao hilo. Mwaka mmoja umepita, bila hata wao kulipwa pesa wanazostahili. Inachukua mashamba ya raia kwa nguvu ili kujenga nyumba ambazo hazitawasaidia. Imewasaliti wenyeji wa eneo hili baada ya kuipigia kura kwa wingi!” akasema Bi Wamuchomba.
Kauli ya mbunge huyo inajiri siku chache, baada ya viongozi kadhaa kutoka eneo hilo kudai serikali imelitelekeza eneo hilo, kwa kuondolea ufadhili baadhi ya miradi iliyokuwa ikiendeshwa na serikali ya Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta.
Viongozi hao kutoka chama cha Jubilee (JP) walisema kuwa ‘ahsante’ ambayo serikali ya Kenya Kwanza imewapa wenyeji wa Mlima Kenya ni kuwatenga kimaendeleo, kuwahangaisha vijana wake na kutotimiza ahadi ilizotoa kwao wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, 2022.
Wakiongozwa na bloga Pauline Njoroge, walisema wataanzisha kampeni kali kulikomboa eneo hilo kutoka mikononi mwa “hadaa ya Kenya Kwanza”.
“Ukweli ni kuwa, fedha zote zilizokuwa zimetengewa miradi muhimu, kama vile barabara ya Mau Mau zimeelekezwa kwingineko. Huu ni mradi mkubwa ambao ikiwa ungekamilika, ungewasaidia sana wakazi wa kaunti hii za Nyeri, Kiambu, Murang’a na Nyandarua. Hata hivyo, ulisimamishwa kwani wale watakaofaidika ni wakazi wa Mlima Kenya,” akasema Bi Njoroge, ambaye pia ndiye Naibu Katibu wa Mipango katika chama hicho.
Bi Njoroge alitoa kauli hiyo mjini Ruiru, Kaunti ya Kiambu, ambako alikuwa ameandamana na wabunge wa zamani Peter Mwathi (Limuru), Jude Jomo (Kiambu) kati ya wengine.
Wanasiasa wengine ambao wamejitokeza kudai eneo hilo limetengwa na serikali ya Rais Ruto ni aliyekuwa gavana wa Kiambu, Bw William Kabogo, aliyesema wakati umefika viongozi kutoka ukanda huo kusimama kidete kuishinikiza serikali kutimiza ahadi ilizotoa kwa wenyeji.