Wandani wa Gachagua sasa wairukia NCIC wakiishutumu kuendesha mapendeleo
SIKU moja baada ya Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) kumwonya aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua dhidi ya kutoa matamshi ya kuchochea chuki, wandani wa mwanasiasa huyo wameigeukia wakidai inatumiwa kumchapa kisiasa.
Wabunge wandani wa Bw Gachagua wanadai tume hiyo inayoongozwa na Kasisi Dkt Samuel Kobia, inatumiwa na Rais William Ruto kuendeleza vita vya kisiasa dhidi ya mwanasiasa huyo huku ikiendesha majukumu yake kwa njia ya mapendeleo.
Kwenye kikao na wanahabari Jumanne jioni, wabunge hao wapatao 10 walidai kuwa ingawa wandani wa Rais Ruto wamekuwa wakitoa matamshi ya uchochezi, NCIC imeamua kumlenga Bw Gachagua “ilhali matamshi yake yalikuwa ya kweli.”
“Matamshi ya Mheshimiwa Gachagua yalilenga kutetea masilahi ya watu wa Mlima Kenya, haswa wale wanaoshikilia nyadhifa kuu serikali. Anapinga njama ya kunyanyaswa kwa watu wetu,” akasema Mbunge wa Gatanga Edward Muriu.
Aliandamana na wenzake; Jayne Kihara (Naivasha), Amos Mwago (Starehe), Wanjiku Muhia (Kipipiri), Onesmus Ngogoyo (Kajiado Kaskazini), Mary Wamaua (Maragua) na maseneta Joe Nyutu (Murang’a) na Dan Maanzo (Makueni).
Mnamo Jumatatu, NCIC, kupitia taarifa iliyotiwa saini na Kasisi Kobia, ilimwonya Bw Gachagua dhidi ya kutoa matamshi ya kuchochea chuki za kikabila kinyume sheria za tume hiyo.
Tume hiyo ilirejelea madai aliyotoa Februari 13, 2025 kwamba Rais Ruto anapanga njama ya kumwondoa afisini Jaji Mkuu Martha Koome “kwa sababu anatoka Mlima Kenya”.
“Tunajua kwamba anapanga kumuondoa Koome afisini kwa kufadhili mashtaka dhidi yake katika JSC. Sasa huyo Rais amezidi. Baada ya kuniondoa afisini sasa amemgeukia Koome….hatutakubali. Na ajue kwamba akimtimua Mama Koome asifike hapa Meru,” Bw Gachagua akasema akiwa katika Kanisa la AIPCA St Joseph KK Garu lililoko eneo bunge la Igembe Kaskazini, kaunti ya Meru.
Lakini sasa wandani wa Bw Gachagua wanahoji hatua ya NCIC kumwonya kwa kutoa matamshi kama hayo ilhali ilimsaza Mbunge wa Webuye Dan Wanyama aliyewahi kutoa kauli iliyohimiza kutengwa kwa Mlima Kenya kimaendeleo.
“Mnamo Januari 19 Mbunge wa Webuye Magharibi Dan Wanyama akiwa katika mkutano uliohudhuriwa na Rais Ruto katika Shule ya Upili ya Wavulana ya Cheptais, alisema kuwa jamii za Mlima Kenya zinapasa kutengwa na jamii zingine. Inasikitisha kuwa NCIC haikumchukulia hatua yoyote kwa sababu yeye ni rafiki wa Ruto. Si hii ni ubaguzi?” Seneta Nyutu akauliza.