Habari za Kitaifa

Simanzi wanafunzi sita wakifariki dunia papo hapo baada ya kugongwa na gari

Na KITAVI MUTUA September 13th, 2024 1 min read

WANAFUNZI sita wa shule walifariki papo hapo mnamo Ijumaa, Septemba 13, 2024 baada ya kugongwa na gari lililokuwa likiendeshwa kwa mwendo wa kasi karibu na soko la Kyoani huko Ikutha, kwenye barabara ya Kitui kuelekea Kibwezi.

Wanafunzi hao ni pamoja na wasichana wawili wa kidato cha tatu na msichana wa kidato cha kwanza waliokuwa wakielekea katika Shule ya Sekondari ya Kyoani mwendo wa saa kumi na mbili na nusu asubuhi.

Wengine watatu ni wanafunzi wa shule ya msingi, mvulana na msichana wa Gredi ya Tatu na msichana wa Gredi ya Sita, wote wa shule ya msingi ya Kyoani.

Watatu kati ya waathiriwa wanatoka familia moja.

Kulingana na ripoti ya awali ya polisi, wanafunzi hao sita walikuwa wakielekea shuleni kutoka nyumbani wakati gari aina ya Toyota Probox lililokuwa likitoka Kibwezi lilipoacha barabara na kuwagonga.

“Gari hilo aina ya Toyota Probox lilikuwa likiendeshwa kutoka upande wa Kibwezi kuelekea Kitui. Lilipofika eneo la Kyoani, dereva aligonga watoto sita waliokuwa wakitembea kwa miguu kando ya barabara wakielekea upande huo huo” ilisema ripoti ya polisi iliyoonekana na ‘Taifa Leo Dijitali.’

Iliongeza kuwa kufuatia tukio hilo, wanafunzi watano wasichana na mmoja mvulana walifariki dunia papo hapo.

Polisi wamemkamata dereva wa Probox ambaye alitoroka eneo la tukio na kuzuilia gari hilo katika Kituo cha Polisi cha Mutomo, huku uchunguzi ukianzishwa.