• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 6:50 AM
2020: Corona ilivyozamisha sekta ya elimu

2020: Corona ilivyozamisha sekta ya elimu

Na WANDERI KAMAU

MIONGONI mwa masuala yaliyoathiriwa sana na mchipuko wa janga la virusi vya corona mwaka huu ni sekta ya elimu.

Mara tu baada ya kisa cha kwanza kuripotiwa nchini mnamo Machi, serikali iliagiza shule zote kufungwa, ili kudhibiti maambukizi yake.

Kutokana na hatua hiyo, karibu taasisi zote za elimu ziliegemea matumizi ya teknolojia na mtandao wa intaneti katika uendeshaji wa masomo.

Ni hali ambayo ilibadilisha namna taasisi hizo ziliendesha masomo mwaka huu, kutoka shule za msingi hadi katika vyuo vikuu.

Ili kuhakikisha kwamba wanafunzi walikuwa wakiendelea na masomo yao kama kawaida, Taasisi ya Kukuza Mitaala Kenya (KICD) ilibuni ratiba maalum ya masomo ili kuwawezesha kufuatilia vipindi vya somo mbalimbali wakiwa majumbani mwao.

Taasisi ilishirikiana na Shirika la Utangazaji Kenya (KBC) na kampuni kama Safaricom kuwafikia wanafunzi walio katika maeneo ya mbali.

Kwenye mkakati huo, KICD ilianza kupeperusha matangazo yake kupitia idhaa za Kiswahili na Kiingereza za KBC na kituo cha televisheni cha Edu Channel.

Kupitia matangazo hayo, wazazi wengi walilazimika kununua redio ama kutumia huduma za mitandao kuwawezesha wanao kufuatili vipindi vya masomo.

Kampuni ya Safaricom nayo ilibuni ushirikiano maalum ka KICD, kwa kuwawezesha wanafunzi kupata maelezo ya elimu kwa njia ya mtandao kwa njia nafuu.

Waziri wa Elimu, Prof George Magoha, alisema serikali ilikuwa ikifanya kila iwezalo kuhakikisha kuwa wanafunzi wanaendelea na masomo yao licha ya vikwazo vilivyojitokeza.

Licha ya mkakati huo, baadhi ya wazazi walilalamika kwamba wanafunzi wengi hawakuwa wakifikiwa na huduma hizo.

Malalamishi yalipozidi, Prof Magoha alitangaza mpango mpya, ambapo walimu walitakiwa kuwafunza wanafunzi kutoka maeneo wanamokaa ili kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo.

Hata hivyo, serikali iliahirisha mpango huo baada ya kupata pingamizi nyingi kutoka kwa wazazi na wadau wengine wa elimu.

Miongoni mwa wale waliojitokeza kueleza kutoridhishwa kwao ni Chama cha Kitaifa cha Walimu (KNUT), Chama cha Walimu wa Vyuo Anuwai (KUPPET), Chama cha Kitaifa cha Wazazi (NPA) kati ya wadau wengine.

Licha ya uwepo wa corona, hilo halikuvizuia vyuo vikuu na taasisi zingine za elimu ya juu kuendeleza masomo kwa wanafunzi.

Taasisi hizo zilivumbua mbinu mbadala za kuwafikia wanafunzi, ambapo zilianza kutumia mitandao.

Kwa mfano, Chuo Kikuu cha Nairobi kati ya vyuo vingine vikuu vya umma vilianza kutumia mfumo wa ‘Zoom’ kuendesha masomo na hata mitihani.

Vyuo hivyo pia vilitumia mfumo huo kuendesha hafla ya kufuzu kwa mahafala wake.

Shule za upili pia zilikumbatia matumizi ya mtandao, kiasi kwamba Mwalimu Mkuu wa Shule ya Upili ya Wasichana ya Othaya, Bi Jane Waceke, alipewa tuzo ya Mwalimu Bora wa Mwaka barani Afrika na Umoja wa Afrika (AU) mwaka huu.

Bi Waceke alipewa tuzo hiyo wiki iliyopita, kwani uvumbuzi wake uliwafaidi wanafunzi wengi hata wale ambao si wa shule anakofunza. Shule hiyo iko katika Kaunti ya Nyeri.

Janga hilo pia liliathiri ratiba na mpangilio wa elimu nchini, hali ambayo kulingana na Wizara ya Elimu, huenda ikaichukua hadi mwaka 2023 kuirejesha ratiba hiyo katika hali ya kawaida.

Kutokana na mpangilio huo mpya, wanafunzi wa Darasa la Nane watafanya Mtihani wa Darasa la Nane (KCPE) Machi 22 hadi Machi 24 mwaka ujao.

Wanafunzi wa Kidato cha Nne nao watafanya Mtihani wa Kidato cha Nne (KCSE) kati ya Machi 25 hadi Aprili 16 mwaka huu.

Kwa kawaida, mitihani hiyo hufanywa katika miezi ya Oktoba na Novemba.

Ni mwaka ambao huenda wanafunzi wasiusahau hivi karibuni, kwani wamekuwa nyumbani kwa zaidi ya miezi kumi. Wanatarajiwa kurejea shuleni kuanzia Januari 4, mwaka ujao.

You can share this post!

CORONA: Shule bado kujiandaa

Tupatane mahakamani, Dorcas Mwende amwambia mamaye Jackline...