• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Alice Wahome adokeza mgombea mwenza wa Dkt Ruto atatoka Mlima Kenya

Alice Wahome adokeza mgombea mwenza wa Dkt Ruto atatoka Mlima Kenya

Na SAMMY WAWERU

MBUNGE wa Kandara Alice Wahome amedokeza mgombea mwenza wa Naibu Rais William Ruto atatoka katika jamii ya Mlima Kenya.

Dkt Ruto ni kati ya viongozi na wanasiasa walioeleza azma yao kumrithi Rais Uhuru Kenyatta mwaka 2022 na kulingana na Bi Wahome atakayesaidia Dkt Ruto kupeperusha bendera ya urais atatoka eneo la Kati ya Kenya.

“Jamii ya Mlima Kenya ina idadi ya juu ya wapigakura, si siri ninahakikishia taifa Dkt Ruto atateua mgombea mwenza kutoka eneo hilo,” akasema mbunge huyo.

Alisema hayo kwenye mahojiano na runinga moja inayopeperusha matangazo yake kwa lugha ya Gikuyu (Inooro).

Kauli ya Wahome imejiri kipindi ambacho imekuwa ikisemekana yapo mazungumzo na kiongozi wa ODM Raila Odinga kupitia Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya ya kujadili uwezekanao wao kuunda mrengo wa kisiasa.

Naibu Rais hata hivyo alipuuzilia mbali madai hayo, akisema si mara ya kwanza yeye kukutana na Bw Oparanya kuzungumzia miradi ya maendeleo.

“Dkt Ruto ndiye Naibu Rais Kenya na ana haki kujadili mikakati ya kuboresha nchi na viongozi wenye maono. Ninachoelewa kumhusu hana haja na miungano ya kikabila, ila muungano utakaoleta Wakenya na mahasla pamoja, waimarike kimaisha na kimaendeleo,” Bi Wahome akasema.

Itakumbukwa kwamba katika uchaguzi mkuu wa 2007, Dkt Ruto na Bw Odinga walikuwa kwenye mrengo mmoja wa kisiasa, ambapo kiongozi huyo wa ODM alitoana kijasho na Rais (Mstaafu) Mwai Kibaki.

Machi 2018 Rais Kenyatta na Bw Odinga walitangaza kuzika tofauti zao za kisiasa, kupitia salamu za maridhiano maarufu kama Handisheki.

Kiongozi huyo wa ODM amekuwa akishirikiana kwa karibu na serikali tawala ya Jubilee, hatua ambayo imeonekana kufungia nje Naibu wa Rais, Dkt Ruto katika maamuzi muhimu.

Ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI) iliyoasisiwa na Rais Kenyatta na Bw Odinga na inayopendekeza Katiba ya sasa kufanyiwa marekebisho, imekuwa ikikosolewa na Dkt Ruto.

Wandani wa Odinga wamedai kuna njama ya kumfungia nje katika Mswada wa BBI, hatua ambayo imeonekana kuchangia kudorora kwa uhusiano kati ya kiongozi huyo wa ODM na Rais Kenyatta.

You can share this post!

Raila chaguo la Uhuru 2022 – Murathe

Leeds United wanyima Liverpool fursa ya kutinga ndani ya...