• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 10:06 AM
Arati aamriwa afike kortini, Kisii na Nyamira zikiendelea kupigania mji wa Keroka

Arati aamriwa afike kortini, Kisii na Nyamira zikiendelea kupigania mji wa Keroka

NA WYCLIFFE NYABERI 

MAHAKAMA ya Mazingira na Ardhi ya Nyamira imeamuru Gavana wa Kisii Simba Arati kufika mbele yake binafsi Jumanne wiki ijayo ili kesi ambayo alishtakiwa kuhusu ukiukaji wa maagizo ya mahakama isikilizwe.

Gavana Arati na Kaimu Katibu wa Serikali ya Kaunti ya Kisii Robert Ombasa, wanatuhumiwa kwa kukiuka agizo la mahakama kuhusu mpaka wa mji wa Keroka.

Mji huo ulioko kwenye mpaka wa kaunti za Kisii na Nyamira, umekuwa ukizozaniwa na serikali hizo mbili.

Kutafuta suluhu kuhusu hali hiyo, diwani wa Rigoma Nyambega Gisesa (Kaunti ya Nyamira) alifika mahakamani na kuomba mahakama iweke bayana mahali ambapo mpaka halisi uko.

Kesi hiyo iliwasilishwa mbele ya Jaji Mugo Kamau ambaye alitoa uamuzi wake uliotegemea pakubwa ramani za masoroveya kutoka kwa Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC) na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Kulingana na ramani hizo, sehemu ambazo awali zilikuwa zinachukuliwa kuwa ziko Kisii, zilionekana kuwa ni za Nyamira.

Hivyo wakati wa kutoa uamuzi, jaji Kamau alisema serikali za kaunti hizo zinafaa kuzingatia kulikowekwa vigingi vya kuonyesha mpaka huo.

Jaji Kamau alisisitiza kuwa hilo pia linafaa kufuatwa katika ukusanyaji wa kodi na mapato mengine kutoka kwa wafanyabiashara.

Lakini Jumapili iliyopita, kulitokea vurumai katika mji huo unaokua kwa kasi baada ya maafisa wa kutekeleza amri za Kaunti ya Nyamira kujaribu kuwapokonya wafanyabiashara miavuli.

Miavuli hiyo ya rangi ya chungwa, ilikuwa imepeanwa na Bw Arati kuwakinga wafanyabiashara na hali mbaya ya hewa.

Aidha Bw Arati alichapisha picha na jina lake katika miavuli hiyo.

Kilichokera maafisa wa Nyamira ni kwamba kiongozi huyo wa Kisii katika kupena miavuli aliwakabidhi baadhi ya wafanyabiashara wa eneo la chini ambalo katika uamuzi wa majuzi kortini, lilipatikana kuwa la Nyamira.

Kwa kuwa mji huo wa Keroka umegawanywa katikati na barabara kuu ya Kisii-Sotik, wafanyabiashara wa upande mwingine ambao hawakupewa miavuli hiyo walionekana ‘mayatima, hali ambayo ilitajwa kwamba ilichochea moto vurumai hizo.

Ilibidi maafisa wa polisi kutumwa hapo kutuliza joto lililokuwa likipanda.

Kufuatia hayo, Bw Gisesa alirudi tena kortini na kupata maagizo hayo.

“Kwa sababu ya uzito wa suala lililotajwa hapa, kesi hii itatajwa Machi 12, 2024, na washtakiwa wote wafike kortini,” agizo hilo la mahakama lilisema.

Mji wa Keroka ulianza kuzozaniwa pindi ugatuzi ulivyoanza, lakini magavana waanzilishi–James Ongwae (Kisii) na marehemu John Nyagarama (Nyamira)–walielewana kiustarabu kugawanya mji huo jinsi barabara ya lami inavyougawa mji huo.

  • Tags

You can share this post!

Hatima ya Dkt Monda kuamuliwa na kamati maalum ya Seneti

Bondia Andiego apigwa breki safari ya Olimpiki

T L