• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 12:26 PM
AstraZeneca yaifaa KNH kwa mashine ya kisasa ya tiba ya kansa ya tezi dume

AstraZeneca yaifaa KNH kwa mashine ya kisasa ya tiba ya kansa ya tezi dume

NA PAULINE ONGAJI

KAMPUNI ya kimataifa ya kutengeza dawa ya AstraZeneca, mnamo Alhamisi ilitoa msaada wa mashine ya kutumia teknolojia ya ultrasound kwa Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) ili madaktari waweze kuchukua sampuli kutoka kwa wagonjwa kupima kansa.

Hatua hii ni sehemu ya mpango wa kampuni ya AstraZeneca kuweka mitambo thabiti ya matibabu ya kansa katika hospitali saba nchini kote, kwa ushirikiano na Taasisi ya Kitaifa ya kansa nchini (NCI Kenya) na chama cha madaktari wa mfumo wa mkojo (KAUS).

Msaada huu unanuia kuangazia hali ilivyo sasa ambapo asilimia 80 ya wagonjwa wa kansa ya tezi dume nchini Kenya, hutambulika kwamba wanaugua muda ukiwa umeyoyoma.

Kansa ya tezi dume ni mojawapo ya aina za kansa zilizokithiri sana miongoni mwa wanaume nchini Kenya, na katika mataifa mengine yaliyoko kusini mwa Jangwa la Sahara.

Aidha, inakadiriwa kwamba visa vipya vya kansa ya tezi dume vinavyogundulika kila mwaka miongoni mwa wanaume kati ya miaka 15-85, vitaongezeka mara tatu zaidi kufikia mwaka wa 2040.

Kwa upande mwingine, idadi ya wanaume wanaoenda hospitalini kufanyiwa uchunguzi kubaini iwapo wanaugua maradhi haya ni asilimia 4.4 pekee, huku uwezekano wa kupimwa ukishuhudiwa kwa wingi miongoni mwa wale walio kati ya miaka 50 na 54.

“Kwa kuimarisha uwezo wa mifumo yetu ya afya kukabiliana na changamoto ya maradhi ya kansa, tunazipa jamii uwezo wa kutafuata huduma bora za matibabu,” alisema Dkt Elias Melly, Afisa Mkuu mtendaji katika Taasisi ya kitaifa ya kansa nchini.

Kulingana na Pelin Incesu, Naibu Afisa Mkuu wa kampuni ya AstraZeneca eneo la Afrika na Mashariki ya Kati, kuwezesha ufikiaji wa teknolojia inayowezesha utambuzi wa mapema wa maradhi haya, unanuiwa kuimarisha ubora wa matibabu ya kansa barani.

Hospitali saba nchini kote ambazo zimepangiwa kupokea mtambo huu wa ultrasound biopsy kufikia mwisho wa mwaka ni pamoja na KNH, Hospitali ya mafunzo na rufaa ya Chuo Kikuu cha Moi (Eldoret), Hospitali ya mafunzo, rufaa na utafiti ya Chuo Kikuu cha Kenyatta (Nairobi), Hospitali ya mafunzo na rufaa ya Jaramogi Oginga Odinga (Kisumu), Hospitali ya mafunzo na rufaa ya Coast General (Mombasa), Hospitali ya mafunzo na rufaa ya Meru (Meru), na Hospitali Kuu ya mafunzo na rufaa ya Kaunti ya Kakamega (Kakamega).

Pindi mtambo wa ultrasound biopsy machine utakapokuwa tayari, chini ya mpango huu, hospitali ya KNH pia itapokea msaada wa mitambo ya reusable biopsy guns na vifaa 10,000 maalum vya kutambua maradhi ya kansa ya tezi dume kupitia vipimo vya damu.

  • Tags

You can share this post!

Lami: Hatimaye Lamu Mashariki yafikiwa

Kocha Ten Hag apumua baada ya Manchester United kutandika...

T L